KADRI siku zinavyosonga mbele, ndivyo ajali za barabarani
zinavyoongezeka na kusababisha vifo na majeruhi wengi, ambao wamepata
ulemavu.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Kikosi cha Usalama Barabarani
kwa kipindi cha miezi mitatu kati ya Januari hadi Machi mwaka huu,
ilionesha kuwa jumla ya ajali 2,443 zilitokea, sawa na wastani wa ajali
814 kwa mwezi mmoja.
Ripoti hiyo ilisema kuwa kuna ongezeko la ajali 327 katika kipindi
cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, ikilinganishwa na ajali 2,116
zilizotokea mwaka jana katika kipindi kama hicho. Pia idadi ya majeruhi
imeongezeka kutoka 2,363 kwa mwaka jana hadi kufikia 2,371 katika
kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.
Uzembe na ukiukwaji wa sheria na kanuni za barabarani ni miongoni mwa
mambo yanayosababisha ajali hizo, zinazokatisha maisha ya watu na
kupunguza nguvu kazi ya taifa. Mfano inadaiwa kuwa utani wa madereva,
ndiyo uliosababisha ajali iliyotokea Maweni tarafa ya Kintinku wilaya ya
Manyoni mkoani Singida juzi na kusababisha vifo vya watu 30 na kujeruhi
wengine 48.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka anasema ajali
hiyo ilihusisha mabasi mawili, mali ya Kampuni ya City Boys, ambapo moja
lilikuwa likitokea Kahama na lingine Dar es Salaam. Anasema mashuhuda
wanaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni madereva wa mabasi hayo mawili,
kutaniana kwa kuyumbusha magari yao wakati walipokutana hapo.
Madereva hao walikuwa wanachezeana kwa staili ile ya kufanya madoido
barabarani ; na katika utani huo deveva wa basi lililokuwa linatokea Dar
es Salaam, alishindwa kulidhibiti hivyo kwenda kumgonga mwenzake,
aliyekuwa anatokea Kahama.
Kwa hakika utani huo uliosababisha watu 30 kupoteza maisha na wengine
kujeruhiwa vibaya, hauvumiliki na haukubaliki hata kidogo. Gazeti hili
linaungana na ndugu, jamaa na marafiki, kuomboleza vifo vya abiria
waliopoteza maisha kwa kuuliza ajali hizi ni mpaka lini?
Tunaomba Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na wadau mbalimbali, kutilia mkazo
suala hili la ajali kwa kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu wake
ipasavyo.
Serikali ifuatilie kwa karibu kuhusu madai ya madereva ili
kuhakikisha kuwa wanapewa mikataba ya kazi na stahili zao ili kuepuka
kuajiri watu wasiokuwa na sifa. Wamiliki wa magari nchini wanatakiwa
kutumia huduma bora za utengenezaji wa magari ili kuondokana na kero ya
kuibiwa vifaa vya magari na utengenezaji wa magari kwa kiwango cha
chini, jambo linalochangia ajali za barabarani.
Utengenezaji mzuri wa magari, unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
ajali za barabarani. Kikosi cha Usalama Barabarani kinatakiwa
kuharakisha utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuzuia makosa ya
barabara kwa kushirikiana na wadau wengine, kama Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano na Sumatra.
Kikosi cha Usalama Barabarani kiongeze faini za barabarani na kwa
kushirikiana na wadau wengine, kiongeze alama na michoro ambayo
itasaidia kupunguza makosa na ajali za barabarani. Elimu itolewe kwa
madereva ili wajifunze kufuata na kuheshimu sheria za usalama
barabarani, kwani baadhi ya ajali zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa
madereva kutoheshimu sheria hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment
karibu kwa maoni