0
KADRI siku zinavyosonga mbele, ndivyo ajali za barabarani zinavyoongezeka na kusababisha vifo na majeruhi wengi, ambao wamepata ulemavu.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kipindi cha miezi mitatu kati ya Januari hadi Machi mwaka huu, ilionesha kuwa jumla ya ajali 2,443 zilitokea, sawa na wastani wa ajali 814 kwa mwezi mmoja.
Ripoti hiyo ilisema kuwa kuna ongezeko la ajali 327 katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, ikilinganishwa na ajali 2,116 zilizotokea mwaka jana katika kipindi kama hicho. Pia idadi ya majeruhi imeongezeka kutoka 2,363 kwa mwaka jana hadi kufikia 2,371 katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.
Uzembe na ukiukwaji wa sheria na kanuni za barabarani ni miongoni mwa mambo yanayosababisha ajali hizo, zinazokatisha maisha ya watu na kupunguza nguvu kazi ya taifa. Mfano inadaiwa kuwa utani wa madereva, ndiyo uliosababisha ajali iliyotokea Maweni tarafa ya Kintinku wilaya ya Manyoni mkoani Singida juzi na kusababisha vifo vya watu 30 na kujeruhi wengine 48.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka anasema ajali hiyo ilihusisha mabasi mawili, mali ya Kampuni ya City Boys, ambapo moja lilikuwa likitokea Kahama na lingine Dar es Salaam. Anasema mashuhuda wanaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni madereva wa mabasi hayo mawili, kutaniana kwa kuyumbusha magari yao wakati walipokutana hapo.
Madereva hao walikuwa wanachezeana kwa staili ile ya kufanya madoido barabarani ; na katika utani huo deveva wa basi lililokuwa linatokea Dar es Salaam, alishindwa kulidhibiti hivyo kwenda kumgonga mwenzake, aliyekuwa anatokea Kahama.
Kwa hakika utani huo uliosababisha watu 30 kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya, hauvumiliki na haukubaliki hata kidogo. Gazeti hili linaungana na ndugu, jamaa na marafiki, kuomboleza vifo vya abiria waliopoteza maisha kwa kuuliza ajali hizi ni mpaka lini?
Tunaomba Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na wadau mbalimbali, kutilia mkazo suala hili la ajali kwa kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu wake ipasavyo.
Serikali ifuatilie kwa karibu kuhusu madai ya madereva ili kuhakikisha kuwa wanapewa mikataba ya kazi na stahili zao ili kuepuka kuajiri watu wasiokuwa na sifa. Wamiliki wa magari nchini wanatakiwa kutumia huduma bora za utengenezaji wa magari ili kuondokana na kero ya kuibiwa vifaa vya magari na utengenezaji wa magari kwa kiwango cha chini, jambo linalochangia ajali za barabarani.
Utengenezaji mzuri wa magari, unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za barabarani. Kikosi cha Usalama Barabarani kinatakiwa kuharakisha utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kuzuia makosa ya barabara kwa kushirikiana na wadau wengine, kama Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Sumatra.
Kikosi cha Usalama Barabarani kiongeze faini za barabarani na kwa kushirikiana na wadau wengine, kiongeze alama na michoro ambayo itasaidia kupunguza makosa na ajali za barabarani. Elimu itolewe kwa madereva ili wajifunze kufuata na kuheshimu sheria za usalama barabarani, kwani baadhi ya ajali zimekuwa zikisababishwa na uzembe wa madereva kutoheshimu sheria hizo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top