0
 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

WATU wawili akiwemo raia wa Congo, Jean Bishikwabo (48) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matano likiwemo la utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh bilioni moja.
Washitakiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya mahakimu wawili tofauti ni Bishikwabo na mfanyabiashara Nagma Mohammed (53). Bishikwabo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Respicius Mwijage na kusomewa mashitaka mawili na Wakili wa Serikali Diana Lukondo.
Ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 2015 na Januari mwaka huu Dar es Salaam, alijipatia Dola za Marekani 700, 000 kutoka katika Kampuni ya Nzuri Trade Limited kwa madai ya kusambaza tani 1,710 za korosho kutoka wilaya ya Masasi, Mtwara hadi kwenye kampuni hiyo ya Nzuri, jambo ambalo alijua hawezi kulifanya.
Katika shitaka la utakatishaji fedha, inadaiwa alifanya muamala wa dola za Marekani 700,000 ambazo zilitokana na fedha haramu za kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuzitakatisha kupitia akaunti yake iliyopo Benki ya Biashara ya Afrika kisha kuzitoa fedha hizo hali akijua ni kosa.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayomkabili hayana dhamana. Kesi itatajwa tena Agosti 25, mwaka huu. Mohammed alisomewa mashitaka matatu, likiwemo la kuendesha shughuli za kimawasiliano kutoka nje ya nchi na kuisababishia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya Sh milioni 203.9.
Mohammed alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri na Wakili wa Serikali Adolf Mkinini akidaiwa, kati ya Mei na Julai 20, mwaka huu katika eneo la Upanga Dar es Salaam aliendesha shughuli hizo kupitia Mkongo wa taifa bila kuwa na kibali cha TCRA.
Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Mei 19 na Julai 20, mwaka huu katika maeneo ya Upanga Dar es Salaam, alikwepa kulipa kodi wakati akifanya shughuli hizo za mawasiliano kupitia Mkongo wa taifa.
Aidha, inadaiwa Mei 19 na Julai 20, mwaka huu akiwa hana kibali alifanya shughuli hizo kwa kutumia mtambo wa GSM VOIP Gateway na kuisababishia serikali hasara hiyo.
Baada ya kusomewa mashitaka, Hakimu Mashauri alisema mshitakiwa huyo hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka. Wakili Mkini alidai kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top