0


WATU watatu wamefariki dunia kwa matukio mawili tofauti Manispaa ya Morogoro wakiwamo wawili waliogongwa na basi la abiria na mwingine, Godwin Salvatory kupigwa risasi na majambazi kwa bastola wakiwa wamepakizana katika pikipiki kisha kupora Sh milioni 3.5 za mfanyabiashara wa kike, Teddy Nestory.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti, la kwanza la uporaji wa kutumia silaha lilitokea saa tatu na robo usiku katika eneo la Kihonda Bima katika Manispaa ya Morogoro.
Alisema watu wawili wanaume wasiofahamika wakitumia usafiri wa pikipiki aina ya Boxer wakiwa na silaha aina ya bastola walimvamia, Teddy Nestory (32) mfanyabiashara na mkazi wa Kihonda Bima akiwa anarudi nyumbani kwake.
Alisema majambazi hao walifyatua risasi iliyomjeruhi Salvatory na kumpora fedha Sh milioni 3.5 na simu saba za aina mbalimbali zilizokuwa katika mkoba na kutokomea kusikojulikana.
Kaimu Kamanda wa Polisi alisema baada ya majeruhi huyo kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa matibabu, alifariki dunia siku moja baadaye Agosti 9, alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini na kwamba jitihada za kuwatafuta watuhumiwa hao zinaendelea.
Katika tukio la pili, alisema katika eneo la Kasanga Darajani katika barabara kuu ya Iringa – Morogoro, Manispaa ya Morogoro ilitokea ajali iliyohusisha gari lenye namba za usajili T 988 CDC aina la Eicher mali ya Kampuni ya Islam Bus Service lililokuwa linaendeshwa na Twaha Mponzi (35) mkazi wa Kihonda likiwa linatokea Ifakara, Kilombero kwenda mjini Morogoro.
Alisema basi hilo liligonga pikipiki yenye namba za usajili MC 164 BGE aina ya Haojue iliyokuwa ikiendeshwa na Jumanne Mussa (44) mkulima na mkazi wa Madaganya ikitokea Kasanga kuingia barabara kuu ya Iringa- Morogoro akiwa amempakia Levanus Leo (37) mkulima na mkazi wa Mindu.
Mussa na abiria wake walikufa papo hapo. Imeelezwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa pikipiki kuingia barabara kuu bila kuchukua tahadhari.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top