Benny
Mwaipaja-WFM, Kyela
KATIBU Mkuu Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali
inathamini mchango wa sekta ya biashara katika kukuza uchumi na maendeleo ya
nchi hivyo itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
Prof. Mkenda
amesema hayo wilayani Kyela Mkoani Mbeya, wakati ujumbe wa Serikali ukiongozwa
na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban,
ulipotembelea mpaka wa Tanzania na Malawi-Kasumulu, ili kujionea utendaji kazi
wa Idara ya Forodha na Uhamiaji katika mpaka huo wa Kasumulu/Songwe.
Amesema kuwa Serikali
inapohimiza ulipaji na kusimamia ulipaji kodi haina maana kwamba inawachukia
wafanyabiashara, bali inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa na
kutoa wito kwa idara za Serikali zilizoko Mipakani kuboresha mazingira ya
utoaji huduma ili kurahisisha biashara.
“Tunatakiwa
kuondoa vikwazo vya ufanyaji biashara ikiwemo ucheleweshaji wa mizigo
inayovushwa katika mipaka yetu kwa kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa Bandari
ya Dar es Salaam na kuzivutia nchi nyingi zaidi kutumia Bandari hiyo” Aliongeza
Profesa Mkenda
Amewaonya
watendaji wa Serikali walioko katika mipaka yote ya nchi, kuacha kufanyakazi
kwa mazoea na kusisitiza kuwa wale wote watakaoshindwa keendana na kasi ya
Serikali ya Awamu ya Tano ni afadhali wapishe kwa hiari yao.
Kwa Upande wake,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban,
amesema kuwa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifawa miaka Mitano, unahitaji
zaidi ya Shilingi Trilioni 107 na kwamba upatikanaji wa fedha hizo utahitaji
mazingira bora ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo mazingira mazuri ya ufanyaji
biashara mipakani
“Serikali
itazifanyiakazi changamoto mlizozisema kama vile upungufu wa wafanyakazi,
vitendeakazi na nyumba za watumishi, lakini wito wangu kwenu muendelee
kufanyakazi kwa pamoja, mshirikiane kwa kuongeza nguvu ili kuongeza mapato ya
Serikali” alisisitiza Bi. Amina Khmis Shaaban
Naye Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, amelitaka
jeshi la polisi hususan kikosi cha usalama barabarani kupunguza urasimu wakati
wa kutekeleza majukumu yao wanapokutana na magari yaendayo masafa marefu nje ya
mipaka ya Tanzania, wasiyacheleweshe njiani bila sababu za msingi.
Kwa upande
mwingine, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Qandiyay
Akonaay, ameeleza kuwa TRA imeanzisha mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mizigo
inayosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwenda nchi jirani, hatua
ambayo imeboresha kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mizigo na kwamba hatua
hiyo pia imeongeza mapato ya kodi ya Serikali
Post a Comment
karibu kwa maoni