Mwandishi wa habari Lodrick Ngowi amewashukuru wazazi wake na wote waliomsaidia kufika hapo alipo baada ya kuchaguliwa kama mpiga picha bora wa mwaka 2016 katika tuzo za Umahiri wa uandishi wa habari (EJAT).
Tuzo hizo, ambazo huhusisha waandishi wa habari wa magazeti, redio, luninga, wapiga picha na wachora vibonzo, limefanyika Aprili 29, jana jijini Dar es Salaam.
Mchujo wa awali ulifanyika Aprili 6 na 13, mwaka huu Bagamoyo, mkoani Pwani.
Wateule hao walichuana kuwania tuzo hizo katika vipengele 19, ikiwa ni pamoja na tuzo ya uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha, michezo na burudani, afya, kilimo na biashara na biashara ya kilimo, elimu, uandishi wa habari na uchambuzi wa matukio.
Nyingine ni habari za utalii na uhifadhi, afya ya uzazi kwa vijana, manunuzi ya umma, kodi na ukusanyaji mapato, habari za uchunguzi, data na haki za binadamu na utawala bora, VVU na Ukimwi, jinsia, wazee na watoto na kundi la wazi, mpiga picha bora za runinga, magazeti na mchora katuni bora.
Kwa mwaka huu mwitikio ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo jumla ya waandishi 810 waliwasilisha kazi zao kutoka 568.
Pamoja na kujitokeza kwa idadi kubwa ya kazi zilizowasilishwa, idadi ya kazi zilizopitishwa imeshuka kutoka 84 mwaka jana hadi 66 mwaka huu.
Tuzo za EJAT huandaliwa kila mwaka kwa ushirikiano baina ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Tasisi ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa).
Wengine ni Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), HakiElimu, AMREF, ANSAF, Best-Dialogue na SIKIKA.
Post a Comment
karibu kwa maoni