Jeremy Meeks, ambaye wakati mmoja alijizolea sifa za kuwa "mhalifu mtanashati zaidi duniani", amezuiwa kuingia Uingereza.
Mwanamitindo huyo alivuma sana mtandaoni mwaka 2014 picha yake ilipopakiwa kwenye mtandao.
Taarifa zinasema alijaribu kuingia Uingereza kwa shughuli za kikazi.
Maafisa wa uhamiaji walimzuia Jumanne katika uwanja wa ndege wa Heathrow, London na tayari amesafirishwa kurejeshwa Marekani.
Maafisa wa wizara ya mambo ya ndani wameambia BBC kwamba wanafahamu kuhusu kisa hicho, lakini hawawezi kuzungumzia kisa cha mtu binafsi.
Hata hivyo, kifungu 320 cha sheria za uhamiaji za Uingereza kinasema maafisa wa uhamiaji uwanja wa ndege au mpakani wanaweza kumzuia mtu yeyote ambaye amefungwa jela kati ya miezi 12 na miaka minne kuingia Uingereza.
Mtu kama huyo hata hivyo hawezi kuzuiwa miaka 10 baada yake kumaliza kutumikia kifungo.
Sheria hiyo ni miongoni mwa masharti mengine yanayoweza kutumiwa kuzuiwa watu waliofungwa jela mataifa ya nje kuingia Uingereza.
Jeremy Meeks alishtakiwa kosa la kuwa na bunduki 18 Juni 2014 na akafungwa jela hadi Machi mwaka jana.
Awali, alikuwa ametumikia kifungo cha miaka tisa kwa kosa la wizi kuanzia 2002 hadi 2011.
Jeremy amekuwa akitafutwa sana na kampuni za mitindo ya amvazi.
Meneja wa Jeremy, Jim Jordan, ameambia Daily Mail kwamba mwanamitindo huyo alikuwa amebeba stakabadhi zifaazo pamoja na barua kutoka kwa afisa wa kumfuatilia mfungwa anayetumikia kifungo cha nje.
Jeremy anadaiwa kutia saini mkataba na kampuni ya White Cross Management siku chache baada ya kuondoka jela mwaka jana.
Alishiriki maonesho ya mitindo mara ya kwanza Wiki ya Mitindo ya New York mwezi Februari.
Picha yake iliyopakiwa na polisi wa Stockton ukurasa wao wa Facebook 2014, imependwa zaidi ya mara 101,000 na kusambazwa mara 12,600.
Post a Comment
karibu kwa maoni