SERIKALI ya Norway
imeipatia Tanzania msaada wa Dola Milioni 10 za Marekani kupitia programu ya
maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, inayotarajiwa kuanza Mwaka Mpya wa
Fedha- Julai Mosi mwaka huu.
Mpango huo pamoja
na uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Mafuta,
umezinduliwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Borge
Brende, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango na Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo kwa niaba ya
Serikali zao.
Dkt. Mpango
ameishukuru Serikali ya Norway kwa msaada huo mkubwa utakaochangia kuboresha
utendajikazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuijengea uwezo zaidi wa
kitaalamu, miundombinu na vitendeakazi vingine vitakavyo changia kuongeza uwezo
wa Mamlaka hiyo wa kukusanya mapato ya Serikali.
Kwa upande wake,
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana
Pallangyo amesema kuwa hatua ya Serikali ya Norway kuendelea kufadhili programu
ya pili ya Mpango wa kuendeleza Sekta ya Mafuta utaiwezesha Serikali kubobea
katika masuala ya utaalamu wa masuala ya sheria na usimamizi wa sekta hiyo.
Nae Waziri wa
Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Borge Brende amesifu utendaji kazi mahili wa Mhe.
Rais Dokta John Pombe Magufuli wa kupambana na ufisadi na vitendo vya rushwa
pamoja na kuimarisha ukusanyaji kodi, hatua ambayo itaifanya nchi ipige hatua
za maendeleo haraka.
Amesema kuwa
hajawahi kuona nchi yoyote duniani ikiendelea bila kuweka nidhamu na uwajibikaji
serikali pamoja na kutokusanya mapato yake ipasavyo na kuahidi kuwa nchi yake
itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano kufanikisha mipango yake
ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Post a Comment
karibu kwa maoni