Serikali imewashauri wakazi wa
Wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro, kutumia njia mbadala kupata huduma za
kibenki ikiwemo kupitia simu za mkononi yaani (simbanking) ya CRDB na Banking on the Wheel ya NMB iliyoko
Mlimba kwa kipindi hiki ambacho mchakato wa kufungua matawi rasmi ya benki
unaendelea.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma
na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Malinyi Dkt. Hadji Hussein Mponda (CCM),
aliyetaka kujua ni lini huduma rasmi za kibenki zitaanzishwa katika wilaya ya
Malinyi ama kama kulikuwa na mpango wa taasisi za fedha kuanzisha huduma za
matawi ya benki yanayohamishika (mobile banking) wilayani humo.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, wilaya ya Malinyi ni moja ya wilaya ambazo
zinanufaika na mfumo wa utoaji huduma kupitia mawakala wa Fahari Huduma
(Malinyi SACCOS na Zidua Waziri Shop)
zinazoendeshwa na benki ya ‘CRDB Bank’ ambapo wateja wanapata huduma za kibenki
ikiwemo kufungua akaunti, kuweka na
kuchukua fedha, kuomba mikopo na kupata ushauri wa huduma za kifedha.
“Gharama
za kuanzisha na kuendesha tawi kuwa kubwa Benki ya NMB na CRDB zinaendelea na
upembuzi yakinifu kwa ajili ya kufungua tawi katika wilaya ya Malinyi utakaotoa
mwelekeo wa kufungua tawi au la, kwa sababu Tawi linatakiwa liwe endelevu na
kujiendesha kwa faida”. Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wananchi wa Tanzania kupata
huduma za kibenki karibu na maeneo yao na kwamba huduma hizo lazima ziwe na faida kwa pande
zote yaani kwa mabenki na wateja pia.
Aidha
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa mabadiliko ya mfumo wa fedha nchini ya mwaka 1991,
yaliitoa Serikali katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za mabenki
nchini ili kuruhusu ushindani huru na kuwezesha kuboresha huduma katika sekta ya fedha.
Katika
swali la nyongeza Mbunge wa Malinyi Dkt. Hadji Hussein Mponda (CCM), alitaka
kujua namna Jeshi la polisi linavyoweza kuwasaidia wakazi wa wilaya hiyo wanaotembea
na fedha nyingi kufuata huduma za kibenki mbali na wilaya hiyo ili wasipoteze
mali zao.
Akijibu
swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba amesema kuwa
Serikali imeendelea kuimarisha usalama katika maeneo hayo ili kuweka ushawishi
kwa Taasisi za kifedha kuweza kufungua mabenki ili kupunguza changamoto ya
huduma za kibenki.
Mwisho
Post a Comment
karibu kwa maoni