0
Rais Dk John Pombe Magufuli ameibua mjadala kufuatia uteuzi wa Mama Anna Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro nafasi iliyoachwa wazi na Said Mecky Sadick.
Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM taifa amemteua mama huyo ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo.
Mama Anna pia alikuwa ni mgombea wa urais wa ACT Wazalendo kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 huku akishika nafasi ya tatu katika matokeo ya uchaguzi mkuu.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mama Anna Mghwira
Ibara ya 61(1) ya katiba ya Tanzania inasema mkuu wa mkoa atakuwa ni kiongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Ibara ya 61 (2) inasema Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
Ibara ya 61(4) inasema kuwa, bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za Mkuu wa Mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.
Aidha kwa mujibu wa sheria ya Serikali za Mitaa na Tawala za mikoa ya mwaka 1984, mkuu wa mkoa ndiye mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa.
Katiba ya Chama cha Mapinduzi inasema kwamba mkuu wa mkoa ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ya Chama cha Mapinduzi.
Katika Mazingira kama haya mama Anna Mghwira atapaswa kuhamia Chama cha Mapinduzi ili kwendana na mfumo unao waongoza wakuu wa mikoa nchini.
Mkuu wa mkoa anatambuliwa kikatiba kama mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM taifa.
Katiba ya CCM Ibara ya 91 inasema mkuu wa mkoa wa ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM wa mkoa.
Katika mzungumzo yake na vyombio vya habari  kiongozi huyo wa chama cha ACT Wazalendo  alisema kwamba iwapo atateuliwa na rais Magufuli katika nafasi yoyote yupo tayari.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top