
MSAJILI wa Vyama vya Siasa ametoa sababu
za kukataa tangazo la kufukuzwa uanachama kwa wabunge wawili wa Chama
cha Wananchi (CUF) - Magdalena Sakaya na Maftaha Nachuma.
Akizungumza na gazeti la Nipashe jana,
Jaji Francis Mutungi alisema taarifa iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Sharif Hamad juu ya kuwavua uanachama wabunge hao
haitambui kwa sababu haikuwasilishwa na mtu mwenye dhamana ndani ya
chama hicho.
Jaji Mutungi alisema ofisi yake
inamtambua Maalim Seif, lakini yeye anaheshimu taarifa ya kukaimu
ukatibu mkuu iliyowasilishwa katika ofisi yake na CUF haijatenguliwa na
chama hicho.
Jaji Mutungi alisema taarifa
iliyowasilishwa na Maalim Seif ya kuwavua uanachama wabunge hao ilipaswa
kuwasilishwa na mtu mwenye dhamana ya majukumu ya Katibu Mkuu au
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ambao ni Magdalena Sakaya au Profesa Ibrahim
Lipumba au wawakilishi wao waliopewa idhini.
Jaji Mutungi alisema kwa mujibu wa
katiba ya CUF ibara ya 80 (1) kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Taifa
kinaweza kuitishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa au Mwenyekiti wa Chama
Taifa ambaye kwa sasa ni Profesa Lipumba.
"Kwa mujibu wa maelezo niliyotoa kuhusu
suala la Magdalena Sakaya kukaimu shughuli za Katibu Mkuu basi kwa
mantiki hiyo na kwa mujibu wa ibara ya 84(2), Mwenyekiti wa Kamati ya
Utendaji Taifa ya chama chenu kwa sasa ni Magdalena Sakaya," alisema
Jaji Mutungi.
Aidha, Jaji Mutungi alisema kwa mujibu
wa ibara ya 91 (c) vikao vyote vya Baraza Kuu la CUF vinapaswa kuongozwa
na Mwenyekiti wa Taifa ambaye ni Profesa Lipumba.
Jaji Mutungi alisema ofisi yake mpaka
sasa haijapokea barua yoyote kutoka CUF inayotengua uamuzi wa
kumkaimisha ukatibu mkuu, Magdalena Sakaya.
Sakaya ni Mbunge wa jimbo la Kaliua mkoani Tabora na Maftaha ni mbunge wa Mtwara mjini.
Post a Comment
karibu kwa maoni