MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, ameiomba Serikali
kuipatia Mamlaka yake vitendeakazi muhimu ili kukabiliana na vitendo vya
uharamia wa bomba la mafuta katika bahari ya Hindi.
Mhandisi Kakoko ametoa maombi hayo
kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyetembelea bandari hiyo
upande wa mafuta na kuelezwa kuhusu tukio lililotokea juzi ambapo TPA
wamekamata boti moja lilikuwa likitumiwa na wahalifu kuiba mafuta kutoka kwenye
bomba, baharini.
Katika tukio hilo watu wasio
fahamika, wakiwa na mabomu na baadhi ya vilipuzi, walilitelekeza boti lao na
kutoweka kusikojulikana kwa kupigambizi baharini baada ya walinzi wa doria
kuwakurupusha kwa kurusha risasi hewani.
“Tunaomba tupatiwe vitendeakazi kwa
ajili ya kikosi chetu kinachofanyakazi kubwa ya kupambana na uhalifu mbalimbali
bandarini hasa magari ili kukiwezesha kikosi hicho kufanyakazi yake kwa ufanisi”
alieleza Bw. Kakoko
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, ameahidi kuipatia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari vitendeakazi
ambavyo viko ndani ya uwezo wake kama Waziri ili kuongeza udhibiti wa eneo la
maji ya bahari lenye bomba la mafuta.
“Ninawapongenza sana kwa kufanikisha
kuwadhibiti maharamia hao ambao wamekuwa wakitumika kuharibu miundombinu ya
bomba na mafuta na kuharibu mita za kupimia mafuta, nawaahidi kuwatimizia
maombi yenu ya vifaa ambavyo viko ndani ya uwezo wangu” alisema Dkt Mpango’
Alisema kuwa vitendo vinavyofanywa na
wahalifu hao vinakwamisha juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu yake na kusabisha
hasara kwa wenye mafuta na kuikosesha Serikali mapato kutokana na vitendo hivyo
vya kutoboa bomba na kuiba mafuta.
Mbali na kushuhudia boti
lililokamatwa pamoja na vifaa vyake ikiwemo injini na magaloni ya mafuta, Dkt,
Mpango alipewa maelezo kuhusu mchakato unaoendelea wa kufunga mita mpya za
kupimia mafuta (flow meters).
Post a Comment
karibu kwa maoni