SERIKALI imeahidi
kuyafanyiakazi malalamiko ya wamiliki wa shule za binafsi nchini kuhusu kodi
mbalimbali wanazotozwa kwa kuwa Serikali inathamini mchango mkubwa wa taasisi
binafsi za elimu katika mapambano dhidi ya adui ujinga.
Ahadi hiyo
imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati wa
sherehe za mahafali ya kumi ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Baobab,
iliyoko Mapinga, Wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Dokta Kijaji
amesema kuwa tayari Serikali imeondoa baadhi ya kodi kwa shule hizo ikiwemo
kodi ya mabango, Usalama mahali pa kazi-OSHA, Ada ya zimamoto, na kwamba kikosi
kazi kilichoundwa na Serikali kupitia upya kodi zingine zinazoonekana kuwa
kikwazo katika utoaji wa elimu, kinaendelea na kazi na matokeo yake yataonekana
hivi karibuni.
“Niko kwenye
kikosikazi kinachoshughulikia changamoto za kodi kwenye shule za watu binafsi
ninaamini suluhisho litapatikana kutokana na Serikali kuthamini mchango wenu
mkubwa katika kuwapatia vijana wetu elimu” alisema Dkt. Kijaji
Alieleza kuwa
katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2017/2018, suala hilo litazingatiwa na
kuwataka wamiliki wa shule binafsi nchini kuwa watulivu wakati jambo hilo
linafanyiwakazi tena kwa umakini mkubwa.
Awali Mwanzilishi
na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Baobab, Bw. Halfan Swai, pamoja na kuiomba
Serikali ifute kodi mbalimbali wanazotozwa kwa kuwa hawafanyibiashara bali
wanaisaidia Serikali kutoa huduma kwa jamii, ameomba pia isaidie kuangalia viwango vya riba vinavyotozwa na
taasisi za fedha nchini kwa kuwa zinawawekeka katika mazingira magumu
wanapohitaji mikopo ya kuendeleza shule zao.
Wanafunzi 149, (wavulana
14 na wasichana 135) wa Shule hiyo wanaotarajiwa
kuhitimu masomo yao ya kidato cha nne hivi karibuni, wameahidi kufanya vizuri
katika mitihani yao kwa kuwa wameandaliwa vizuri na walimu waliobobea katika
ufundishaji pamoja na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia shuleni
hapo.
Post a Comment
karibu kwa maoni