Waziri wa Mambo ya Nje Nchi, Dkt Augustine Mahiga amekiri Tanzania
imepunguza uhusiano wa kibiashara na nchi ya Korea Kaskazini tangu
mwaka 2014 hivyo Tanzania imeshtushwa baada ya kutajwa miongoni mwa nchi
ambazo zimechunguzwa na Umoja wa Mataifa.
Akizungumza
leo na wanahabari jijini Dar es salaam , Mh. Waziri amesema licha ya
uhusiano uliokuwepo awali, lakini tangu mwaka huo Tanzania imepunguza
kabisa uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia ingawa hakuna ugomvi, na
kusema kitendo cha kuhusishwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi
hiyo kimeishtua serikali
"Hatuna ugomvi na Korea Kaskazini,
lakini kitendo chao cha kutengeneza silaha za kuangamiza siyo kizuri
kwa heshima na usalama wa dunia. Ndiyo maana tukaanza kuchukua hizo
hatua za kupunguza mahusiano tangu 2014," amesema
Mh. Mahiga amefafanua kuwa awali
uhusiano wa kibiashara ulikuwepo kabla ya vikwazo vilivyowekwa hivi
karibuni na Baraza la Umoja wa Mataifa.
Inadaiwa kuwa Tanzania na Uganda ni
miongoni mwa baadhi ya nchi zinazochunguzwa na Umoja wa Mataifa kwa
tuhuma za kwenda kinyume na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.
Hata hivyo ripoti ya uchunguzi huo
ilitolewa Septemba 9, 2017 ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
lilisema linachunguza tuhuma za Tanzania kuingia mikataba ya kijeshi na
Korea Kaskazini inayogharimu dola za kimarekani milioni 12.5.
Pamoja na hayo Waziri Mahiga amesema
kuwa anaelekea katika mkutano wa kawaida wa Umoja wa Mataifa na akiwa
huko atatumia fursa hiyo kujibu tuhuma hizo kwa Baraza la Usalama.
Post a Comment
karibu kwa maoni