0

Hizi ni taka taka zilizosambaa katika kizimba kilichopo pembezoni mwa kiwanja cha Kwaraa mjini Babati.

Wakazi wa mji wa Babati wameiomba Halmashauri kuziondoa mapema taka zinazokusanywa katika vizimba ili kuepuka kuzagaa ovyo kutokana na upepo.
Wafanyabiashara wanaozunguka eneo la kizimba  cha Kwaraa na soko la Darajani kinachokusanya taka kwa muda kabla ya kupelekwa dampo kuu katika kijiji cha Gaduet kata ya Sigino wamesema licha ya kuwaathiri lakini pia linawafukuza wateja wao kutokana na harufu mbaya inayotekea katika taka hizo ambazo zimekuwa zikikaa kwa muda mrefu bila kuondolewa.
Muonekano wa kizimba cha taka Kwaraa,taka hizo zinadaiwa kuwepo hapo zaidi ya wiki sasa.
Akizungumzia hilo katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi jumatatu ya wiki hii katika ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Babati wakati mwenyekiti wa wa Halmashauri Mohamedi Kibiki akifungua baraza hilo ambalo ni la mwisho katika mwaka huu wa 2017 aliitaka idara husika kusimamia hilo ilio kuuweka mji katika hali ya usafi.
Mkuu wa idara ya usafi na Mazingira  na udhibiti wa taka ngumu Halmashauri ya mji wa Babati Faustin Masunga amekiri kuwepo kwa taka hizo kwa muda mrefu huku akisema kinachosababisha ni upungufu wa Madereva  akisema kuwa kwa sasa wanasubiri vibali vipya vya ajira ili kutatua changamoto hiyo.
Masunga ameawataka wakazi wa mji wa Babati kuchangia huduma ya kuzoa taka na kutupa taka katika maeneo husika ili kuepuka kuzagaa ovyo kwa taka taka.
Aidha masunga ameeleza kuwa Halmashauri ina Magari matatu kwa ajili ya kuzikusanya taka na kuzipeleka Dampo kuu ila zoezi la uhakiki lilisababisha kuwakosa madereva wa magari hayo,kwa sasa wanasubiri vibali vya ajira vitoke.
Katika kuhakikisha mji wa Babati unakuwa katika hali ya usafi  hivi karibuni Halmashauri ya mji ilinunua gari la kisasa lenye thamani ya shilingi milioni 200.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top