0

Taarifa mbaya kutoka jijini Arusha leo January 30, 2018 inaeleza kuwa Watu wanne wamefariki Dunia katika kata ya Murieti kwenye eneo la mlima CCM baada ya kuangukiwa na maporomoko ya mawe na kuwafukia ardhini wakati walipokuwa wakichimba mchanga.

Mganga Mkuu wa jiji la Arusha Dr. Saimon Chacha amethibitisha tukio hilo nakusema miili hiyo imeondolewa katika eneo hilo nakupelekwa katika hospitali ya Mount Meru.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo akizungumza na WALTER HABARI ametihibitisha kutokea kwa tukio hilo katika eneo ambalo ni machimbo ya muda mrefu ya changarawe.

Miili ya watu watatu tayari imetambulika ambao ni Yusuph Mohamed Kamwende(35) Athuman Hussein  umri wake haujatambulika na Richard Kishimbo(57).

"Bado  mwili wa marehemu mmoja haijafahamika na tunaomba watu kufika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya mkoa Mount Meru kutambua ndugu zao" alisema  Kamanda.

Hata hivyo, alitoa  wito kwa maafisa madini kwenda mara kwa mara kwenye maeneo ya machimbo ili kutazama usalama wa maeneo hayo ili kuondoa majanga.

"Pale inaonekana ngema moja ilikuwa imelegea sasa wao wakiwa wanachimba changarawe ndipo iliwadondokea na kuwafukia" alisema

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, John Lemanya amesema  wakati watu hao wakichimba, ilisikika mlio wa kuanguka  ngema na waliona wakiangukiwa.

"Wao walikuwa wameingia chini ya ngema na kuanza kukata miamba na ndipo mtikisiko ulitokea na kufanya kumeguka kwa ngema na kuwaangukia"Amesema

Hata hivyo hili ni tukio la pili ndani ya miaka mitatu kutokea ambapo mwaka juzi pia machimbo hayo yalifungwa baada ya kusababisha vifo kutokana na wachimbaji kuangukiwa na ngema.



Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top