Viongozi 18 wa chama cha ACT-Wazalendo kutoka mikoa mbalimbali nchini wamejivua nyadhifa zao na kujiunga na CCM.
Viongozi
hao wamepokelewa jana Januari 17, 2018 mjini Moshi na Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna
Mghwira ambaye hivi karibuni alihamia chama tawala.
Mghwira amewahi kuwa mwenyekiti wa ACT.
Miongoni mwa wanachama hao, wapo waliokuwa wajumbe wa kamati kuu, wenyeviti wa mikoa na makatibu wa ACT.
Pia, viongozi 18 wa Chadema ngazi za kata na vijiji kutoka Wilaya ya Siha nao wamejiunga na CCM.
Akizungumza
baada ya kuwakaribisha, Polepole amesema katika kipindi cha miaka
miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, CCM kimeongeza wanachama
zaidi ya milioni mbili.
"Tukisimamia
haki na heshima kwa watu wote CCM kitatawala milele nchi hii. Kwa
sababu misingi ya chama hiki ni utu. Sasa tunahitaji watu ambao
wanachukizwa na rushwa, ubadhirifu na ubinafsi,” amesema Polepole.
Kwa
upande wake Mghwira amesema siasa bado ina changamoto kubwa na kuwataka
wanasiasa kufanya siasa za kuwaunganisha watu pamoja, si kujenga uadui.
"Nchi
haiwezi kujengwa kwa maneno ya kashfa…,ili tupige hatua kimaendeleo
inatakiwa idadi ya vyama vya siasa ipungue kwa sababu utitiri wa chama
ni mkubwa ikilinganishwa na ukubwa wa nchi yete,” amesema Mghwira.
Aliyekuwa
mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT, Kansa Mbaruku amesema wamechukua maamuzi
hayo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya viongozi waandamizi wa
chama hicho kuhama, akiwemo Mghwira .
Baadhi
ya viongozi hao ni Eva Kaka (mjumbe Kamati Kuu), mwenyekiti wa Mkoa
wa Dodoma Anganile Massawe, Athuman Balozi (mwenyekiti mkoa wa Tabora),
Hamad Nkya (mwenyekiti mkoa wa Kilimanjaro), Godwin Kayoka (katibu wa
mkoa Tabora) na Juma Hamisi (mwenyekiti wazee mkoa wa Singida).
Post a Comment
karibu kwa maoni