Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi amepelekwa mahabusu
katika Gereza la Ruanda mkoani Mbeya baada ya kukosa dhamana katika kesi ya
uchochezi inayomkabili.
Sugu na Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
Emmanuel Masonga wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya leo Januari
16 na kupelekwa mahabusu leo Jumanne Januari 16, baada ya Wakili wa Serikali,
Joseph Pande kuiomba mahakama kuzuia dhamana kutokana na usalama wa washtakiwa
kutokana na kosa walililotenda.
“Kosa walilolitenda washtakiwa ni kutoa maneno ya fedheha
yanayomtaja rais kuwa muuaji hivyo wakiwa nje wanaweza kupata matatizo kwa
wananchi ambao hawajapendezwa na maneno hayo,” alidai Wakili Pande.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite alikubaliana
na ombi hilo ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwaka huu atakapotoa
uamuzi wa dhamana.
Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya uchochezi kwa kutoa lugha
ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, Desemba 30, mwaka jana akiwa katika
viwanja vya mikutano vya shule ya msingi Mwenge iliyopo jijini Mbeya ambapo
Sugu anadaiwa kutamka kuwa rais ni muuaji.
Post a Comment
karibu kwa maoni