0
Image result for MKAASERIKALI imetoa muda wa mwaka mmoja kwa taasisi zake kujiandaa kuhama kwenye matumizi ya mkaa na kuhamia kwenye nishati ya gesi na mkaa mbadala ili kuondokana na uharibifu wa mazingira.
Kauli hiyo ilitolewa  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira January Makamba wakati wa upandaji miti kuendeleza programu ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Alisema miongoni mwa taasisi hizo ni magereza, shule, vyuo na hospitali nchini ambazo zinatumia mkaa kupikia. January alisema ofisi yake inatarajia kutoa waraka na kwamba asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa kupikia na kumuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuandaa mkakati wa kupunguza matumizi ya mkaa nchini.
“Tunazitaka taasisi za umma ziache kutumia mkaa tutatoa tamko hilo rasmi kwa waraka hata wazabuni hawatapata zabuni kama hawatatumia gesi. Kifungu cha 13 cha sheria ya mazingira, waziri mwenye dhamana ya mazingira ana uwezo wa kutoa maelekezo kufanya jambo litakalookoa mazingira,” alisema January.
“Mkaa ni nishati yenye gharama kushinda sehemu yoyote, maisha ya watu wa vijijini yanazidi kuharibiwa kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema. Kwa upande wake, Naibu Waziri wake, Kangi Lugola alisema serikali haitawavumilia wawekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda vinavyotiririsha kemikali za sumu kwa kisingizio cha sera ya Tanzania ya viwanda.
“Serikali haitawafumbia macho watu wote wanaoharibu mazingira kwa kisingizio cha sera ya Tanzania ya Viwanda. Watu wamejisahau sana wanajua wanaweza kuishi bila kutunza mazingira,” alisema Lugola.
Alisema wapo watu binafsi na kampuni wanawekeza katika sekta mbalimbali, lakini wamekuwa hawazingatii utunzaji wa mazingira. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Joseph Malongo alisema awamu ya pili ya zoezi la upandaji miti litafanyika kwenye barabara zote zinazoingia mkoani Dodoma.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, alisema jimbo lake linatekeleza programu ya upandaji miti kwa kila kata na kwamba utunzaji mazingira wao kama viongozi wa kisiasa wameifanya kama ajenda ya kudumu kwenye mikutano yao ili kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema miti 30,000 itapandwa katika maeneo ya chuo hicho huku akihimiza wanachuo kutunza mazingira na kwamba wameunda kikosi kazi cha kudhibiti uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii inayozunguka chuo.
Kadhalika, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Sadiq Murad alisema sera ya viwanda iende sambamba na utunzaji mazingira kwa kuwa viwanda vimekuwa havitunzi mazingira huku akitoa angalizo kwa chuo hicho kuhakikisha miti iliyopandwa inastawi.
Upandaji huo wa miti ni utekelezaji wa kampeni ya Kijanisha Dodoma iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan inayofadhiliwa na Kampuni ya The Network inayoendesha bahati nasibu ya Tatu Mzuka.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top