Balozi
mpya wa Tanzania nchini Sweden, Dk Willibrod Slaa ameapishwa leo
Februari 16, 2018, Ikulu Dar es Salaam na Rais John Magufuli na kuahidi
kuwa utendaji wake utajikita kwenye diplomasia ya uchumi.
Mbali
na Dk Slaa ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Rais Magufuli
pia amemuapisha Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Muhidin Mboweto.
Rais
Magufuli alimteua Dk Slaa kuwa balozi Novemba 23, 2017 na tangu wakati
huo alikuwa akisubiri kupangiwa kituo chake cha kazi.
Dk
Slaa ambaye tangu ajiuzulu wadhifa wake Chadema amekuwa akiishi Canada,
alitangaza kuachana na siasa kutokana na kutofautiana na chama chake
katika kumpokea Edward Lowassa aliyehamia kutoka CCM na baadaye
kupitishwa kuwa mgombea urais kupitia muungano wa Ukawa.
Alisema chama chake hakikutekeleza makubaliano waliyoafikiana ya kuwapokea baadhi ya makada wa CCM akiwamo Lowassa.
Hafla
hiyo fupi ya Ikulu ilihudhuliwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje, Dk Suzan
Kolimba na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili, Jaji Harold Nsekela.
“Tangu
nikiwa mbunge na wewe ukiwa bungeni, tumepigia kelele sana ubalozi wa
kiuchumi na wewe baada ya kuanza mwaka wa pili, umeanzisha mchakato wa
spidi kali katika kila eneo ili kufikisha mahali safari ya kuikuza
Tanzania kiuchumi,” amesema Dk Slaa,
“Katika
ulimwengu wa leo, pamoja na kazi zile nne zilizozoeleka, diplomasia ya
sasa ni ya kiuchumi. Ninakushukuru kwa kunipeleka mahali ambapo naweza
kutoa mchango wangu.”
Dk
Slaa aliahidi kufanya kazi kwa uwezo wake, akili na kwa nafasi yake
yote huku akimwomba Mungu amsaidie kufanikisha dhana ya Tanzania ya
viwanda.
“Natambua
kwamba maendeleo ni safari na safari yoyote unakwenda hatua kwa hatua.
Huwezi kusema unakwenda Mbeya, ukaruka dakika ile ile au sekunde ile ile
ukafika Mbeya. Unapiga hatua moja, ya pili unapanda kituo cha kwanza
cha pili na tatu,” amesema,
“Ahsante Mheshimiwa Rais kwa kuniona, kwa kuniamini na kunipa majukumu haya, naamini sitakuangusha.”
Naye
Balozi Mboweto licha ya kumshukuru Rais Magufuli aliahidi kufanya kazi
kwa uwezo wake wote kwa bidii kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya
utendaji wa serikali.
Akisisitiza diplomasia, Dk Kolimba amewahakikishia mabalozi hao ushirikiano katika kutimiza adhama hiyo.
“Jukumu
kubwa tulilopewa ni kutekeleza diplomasia ya uchumi na kwa nchi ambazo
umewapeleka mabalozi hawa najua watatumia uzoefu walio nao na tutawapa
ushirikiano wa kutosha,” amesema.
“Tunataka
kuwahakikishia mabalozi hawa wawili walioteuliwa leo sisi kama wizara,
tutawapa ushirikiano wa kutosha kwa sababu wao watakuwa sehemu ya
wizara.”
Post a Comment
karibu kwa maoni