Wakazi waishio jirani na
Pori la Akiba la Mkungunero lililoko Wilayani Kondoa mkoani Dodoma, wameiomba
Serikali iwarejeshee eneo la kilometa 12 kuanzia kwenye vijiji vyao kwenda ndani ya Pori hilo ambalo wanadai limechukuliwa
kinyemela na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuathiri maisha yao yanayotegemea
kwa kiasi kikubwa kilimo na ufugaji.
Wakazi wa vijiji vya
Ikengwa, Keikei Tangini, Keikei na Kisondoko, wametoa maombi hayo mbele ya
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala wakati alipofanyaziara
katika vijiji hivyo vinavyozunguka Pori hilo la Akiba ili kutatua mgogoro wa
muda mrefu baina ya Pori hilo na wananchi wanaolizunguka.
Wananchi na viongozi wa
vijiji hivyo wameeleza kuwa uwekaji wa mipaka ya Pori hilo haukuwa shirikishi
na kwamba maeneo makubwa ya vijiji yaliyokuwa yakitumiwa na wananchi kwa
shughuli zao za kilimo, ufugaji na makazi yametwaliwa na kusababisha mgogoro
huo.
Malalamiko mengine ya
wananchi hao ni kunyanyaswa na watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero kwa
kupigwa, kunyang'anywa mifugo yao, na baadhi yao kudai kuumizwa na baadhi ya
wenzao kuuawa kwa risasi na askari wanaolinda Pori hilo.
Kwa Upande wake Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini
Dkt. Ashatu Kijaji, ameiomba Serikali kutumia busara na kurejesha eneo
lililochukuliwa kimakosa kutoka kwa wananchi ili waweze kujiendeleza kiuchumi
na kuishi kwa amani na utulivu.
"Najua wewe ni
mwadilifu ndio maana umeaminiwa na Mhe. Rais, najua utawatendea haki wananchi
wa vijiji hivi ili nao wajione ni wananchi halali katika Taifa lao huru la
Tanzania tukienda hatua kwa hatua bila kuvunja sheria za nchi" alisisitiza
Dkt. Kijaji
Amefafanua kuwa maeneo yaliyochukuliwa
na Pori hilo yalikuwa yakitumiwa na wananchi kwa muda mrefu na kwamba mchakato
wa kupandisha hadhi eneo hilo kutoka Pori Tengefu hadi kuwa Pori la Akiba la
Mkungunero haukuwashirikisha wananchi.
Akijibu Hoja za Wananchi
hao, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, pamoja na kutoa elimu
kuhusu umuhimu wa uhifadhi kwa ustawi na maendeleo ya nchi, aliwahakikishia
wananchi hao kwamba Serikali itatafuta njia ya bora ya kuumaliza mgogoro huo
kwa maslahi ya pande zote mbili, wananchi na Serikali.
"Ni lazima tutafute
mahali ambapo tutabalance, maslahi ya umma na maslahi mapana ya Taifa zima na
niwahakikishie kuwa tutafanyakazi hiyo kwa uadilifu, uzalendo mkubwa, lakini
zaidi kwa kuzingatia maslahi yenu wananchi wenzetu" Alisisitiza Dkt.
Kigwangala.
Awali, Meneja wa Pori
hilo, Emmanuel Birasso, alieleza kuwa mchakato wa kuanzisha Pori hilo la Akiba
Mkungunero ulifuata taratibu za kisheria za uanzishwaji wa mapori ikiwa ni pamoja
na kuwashirikisha wananchi jambo ambalo linapingwa na wananchi hao.
Alieleza kuwa mpaka sasa
takriban kilometa 118 za mpaka wote wa Pori umesimikwa alama za mipaka na
kuwaondoa watu wanaodaiwa kuvamia Pori hilo pamoja na kuimarisha ulinzi na doria.
Post a Comment
karibu kwa maoni