0
Watu 20 wamefariki dunia kwa kipindupindu kati ya  471 waliougua ugonjwa huo mkoani Dodoma tangu Oktoba, 2017.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Charles ameyasema hayo leo Februari 20, 2018 kuwa wilaya zilizoathiriwa na ugonjwa huo ni Bahi, Kongwa, Chamwino na Mpwapwa.

Amesema Mpwapwa imeathirika kwa kiwango kikubwa na ugonjwa huo na kwamba kati ya vifo hivyo 18 vimetokea wilayani humo.
“Oktoba 19 mlipuko wa ugonjwa huo ulijitokeza katika kijiji cha Mlowa Wilayani Chamwino na kusambaa katika Wilaya za Bahi na Kongwa lakini ulidhibitiwa”, amesema.
Hata hivyo, amesema mlipuko huo ulishika kasi tena Desemba mwaka jana katika Wilaya za Chamwino na Mpwapwa ambapo hadi kufikia jana watu 20 walifariki dunia na wengine 471waliugua,” amesema.
Amesema kati ya wagonjwa hao 471, 322 walitokea katika wilaya ya Mpwapwa na kwamba kichocheo kikubwa ni uhaba wa majisafi na salama.
” Wagonjwa wengi katika Wilaya ya Mpwapwa walitokea shambani sababu iliwafanya kuchelewa katika vituo vya kutolea huduma,” amesema.
Amesema hadi kufikia juzi kulikuwa na wagonjwa wapya 10 ambapo kati ya hao wametokea katika Wilaya ya Mpwapwa huku mmoja akitokea katika Wilaya ya Kongwa.
Amesema vijiji 28 vimeathirika na ugonjwa huo katika wilaya ya mpwapwa mkoani hapa.
Amesema wagonjwa waliokuwa katika kambi maalum za ugonjwa huo walikuwa 13 wakati 13 wengine waliruhusiwa kwenda majumbani baada ya matibabu.
Amesema katika jitihada za kuzuia ugonjwa huo mkoa umeongeza jitihada katika elimu ya usafi wa mazingira na pia wamegawa vidonge zaidi ya 250,000 vya kutibu maji.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top