0
Mvutano umeibuka bungeni kati ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Mvutano huo umeibuka leo Mei 9, 2018 baada ya Mchungaji Msigwa kutakiwa kufuta maneno aliyoyazungumza kuhusu utendaji wa Rais John Magufuli  katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19.

Mbunge huyo alianza kuzungumzia kero za maji majimboni, kueleza jinsi wabunge wengi wanavyolalamikia jambo hilo na kubainisha kuwa kama ni suala la uwajibikaji wa Serikali, inapaswa kuundwa tume.

Huku akitolea mfano kukosekana kwa maji ni sawa na wananchi kula uchafu, wakiwemo watalii na huenda wote wakapata ugonjwa wa kipindupindu, Mchungaji Msigwa aliingia katika mvutano huo baada ya kudai kuwa tatizo la maji ili litatuliwe ni mpaka Rais John Magufuli apige simu kwa Katibu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

“Yaani tatizo la maji hadi Rais apige simu kwa katibu wa wizara, aunganishwe na mtendaji wa kijiji, hii inaoyesha mfumo umekwama,” amesema.

Amesema katibu huyo wa wizara amejikita mitandaoni kujibizana na maaskofu badala ya kutafuta ufumbuzi wa maji.

Wakati akiendelea kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alisimama na kusema kwa mujibu wa kanuni ya 64, mbunge hatozungumzia utendaji wa Rais ndani ya Bunge.

“Madaraka aliyopewa Rais ni ya kikatiba, anaweza kusimamia jambo lolote, kwa utaratibu wowote anaoona unafaa kwa muktadha wa Watanzania. Na kanuni zinatufunza tusizungumzie mienendo ya Rais,” amesema Mhagama.

“Tukiacha liendelee kama anavyofanya Mchungaji Msigwa si sawa na tunavunja Katiba, ninaomba aheshimu kanuni ya 64 (1)(e) ya Bunge na kama itakupendeza Naibu Spika hayo anayozungumza afute.”

Baada ya maelezo hayo, Naibu Spika alisimama na kumtaka Mchungaji Msigwa kufuta maneno hayo.

Hata hivyo, Mchungaji Msigwa amesema hajui afute maneno gani jambo ambalo lilimnyanyua tena Dk Tulia, “kama hujui ufute yapi, futa mchango wako wote uliochangia na uanze moja.”

Agizo hilo lilipingwa na Mchungaji Msigwa na kuendelea kuchangia kitendo ambacho Dk Tulia hakukubaliana nacho na kumtaka aketi huku akimuita mbunge mwingine kuendelea na mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top