0
David GoodallMwanasayansi David Goodall, 104, aliyesafiri kutoka Australia hadi Uswizi ili kujitoa uhai amefariki katika kliniki moja nchini Uswizi, shirika linalotetea haki za watu wanaotaka kufa limetangaza.
Mwanaikolojia huyo ambaye pia alikuwa mtaalamu wa mimea hakuwa anaugua lakini alisema aliamua kujitoa uhai kutokana na kudhoofika kwa 'ubora wa maisha yake'.
Bw Goodall alikuwa amezua mjadala kutokana na safari yake ya kutoka Australia kwenda kujitoa uhai.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, alisema alikuwa na "furaha kuhitimisha" maisha yake.
"Maisha yangu yamekuwa dhaifu sana kwa mwaka mmoja hivi uliopita na hivyo basi nina furaha kuyahitimisha," alisema akiwa amezingirwa na jamaa wake kadha.
"Nafikiria, kuangaziwa kwa kisa changu kutachangia kutetea haki za wazee kuruhusiwa kujitoa uhai, jambo ambalo nimekuwa nikitaka."
Alifariki mwendo wa saa sita unusu mchana katika kliniki ya Life Cycle mjini Basel baada ya kudungwa sindano ya Nembutal, kwa mujibu wa Philip Nitschke mwanzilishi wa shirika la Exit International lililomsaidia kujitoa uhai.
"Najuta kufika umri huu," Dkt Goodall alisema mwezi uliopita katika sherehe ya kuzaliwa kwake, katika mahojiano na shirika la utangazaji la Australia.
"Sina raha. Nataka kufa. Sio jambo la kuhuzunisha, kinachohuzunisha ni kwamba mtu anazuiwa kufa."
Ni jimbo moja pekee Australia lililohalalisha kujitoa uhai mwaka jana kufuatia mjadala mkali uliozusha mgawanyiko, lakini ili mtu kuruhusiwa, ni sharti awe anaugua mahututi.
Je ni mataifa gani mengine yanaruhusu kujitoa uhai?
  • Uswizi, ni nchi pekee iliyo na vituo vinavyotoa huduma hiyo kwa raia wa mataifa mengine.
  • Uholanzi, Ubelgiji na Luxembourg zinaruhusu, hata kwa watoto lakini katika hali maalum.
  • Colombia inaruhusu kujitoa uhai kwa hiari wakati mgonjwa akiwa hatibiki.
  • Majimbo sita ya Marekani - Oregon, Washington, Vermont, Montana, California na Colorado - zinaruhusu kwa wagonjwa mahututi wasio tibika.
  • Canada ililifuata jimbo la Quebec kuruhusu hilo mnamo 2016.


Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top