0
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amefafanua kuwa Muswada wa Sheria ya Upatikanaji Taarifa wa mwaka 2016, uliosomwa kwa mara ya pili bungeni, haugusi moja kwa moja tasnia ya habari.
Ameongeza kuwa muswada kwa ajili ya huduma za vyombo vya habari, upo na utawasilishwa bungeni.
Alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati akiunga hoja mkono kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa.
Alisema ameridhishwa na muswada huo, uliofanyiwa kazi kwa miaka kumi, akiwasifu wadau kwa kuutendea haki, kwani licha ya kuchelewa na kuchukua muda mrefu, una ubora na kusema utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania.
Hata hivyo, alisema tofauti na baadhi ya wabunge waliotumia nguvu kubwa kuukosoa wakiamini unagusa moja kwa moja sekta ya habari, Waziri Nape alisema ni vitu viwili tofauti na kwamba wabunge walijichanganya, pengine kwa kuwa hawakuusoma vizuri, lakini Muswada mahsusi kwa ajili ya Huduma za Vyombo vya Habari upo.
“Wabunge wamejichanganya katika hili….kuna Muswada huu wa Upatikanaji wa Taarifa uliodhaniwa unagusa moja kwa moja tasnia ya habari, lakini ndugu zangu niwahakikishie kuna Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari. Huu upo na utaletwa bungeni,” amesema.
Alifafanua kuwa, ingawa wadau wa habari walishirikishwa lakini kamwe hauigusi moja kwa moja tasnia ya habari, huku akisisitiza muswada huo ukipitishwa na kupatikana sheria utaongeza uwajibikaji kwa taasisi za umma kwani wananchi watakuwa na haki za kupata habari.
“Si kweli kwamba unakuja kuvuruga vyombo vya habari na sekta kwa ujumla, hapana. Wanaosema hivyo ni wapotoshaji. Pia wanaopinga Muswada wa Upatikanaji wa Taarifa, hawa wanapinga uwajibikaji na kama hakuna uwajibikaji, ni dhahiri hakuwezi kuwa na maendeleo,” alisema.
“Aidha…Nape leo yuko, kesho hayupo…si sheria yangu.” amesema Nape.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top