MKUU WA WILAYA YA HANDENI, GODWIN GONDWE.
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, ameshangazwa na idara ya elimu msingi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kushindwa kumchukulia hatua aliyekutwa amelewa wakati wa kazi.
Mwalimu huyo, Fikiri Swai wa Shule ya Msingi Kwankonje, anatuhumiwa kufika kazini akiwa amelewa pombe.
Tukio hilo lilitokea juzi shuleni hapo wakati Gondwe alipofika katika mpango wa kusambaza mbegu za mihogo na katika shughuli hiyo, alifika mwalimu huyo na kuanza kusalimia akiwa amelewa chakari.
Kutokana na hali hiyo, Gondwe alitaka kufahamu kama ni mwalimu wa shule hiyo na ndipo alipojibiwa kuwa ndiyo na kuelezwa kuwa hiyo ni tabia yake ya muda mrefu. Pia ilielezwa kuwa ameshachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kusimamishwa kazi.
Baada ya majibu hayo, Gondwe alisema mtumishi wa umma kufika kazini akiwa amelewa au kufanya hivyo muda wa kazi na kwamba kitendo cha mwalimu huyo ni kosa na ameonyesha dharau mbele ya viongozi wa ngazi ya juu ndani ya wilaya.
"Kumbe mmeshamsimamisha sasa kwa nini anakuja shuleni tena akiwa amelewa muda wa kazi? Hamuoni inaleta taswira mbaya kwa wanafunzi kuona hili ni jambo la kawaida? Kwa kweli sijafurahishwa na hili kabisa," alisema Gondwe.
Alipoulizwa sababu ya kulewa pombe muda wa kazi, Mwalimu Swai alisema hali hiyo inatokana na kusimamishwa kazi kwa muda mrefu hivyo kumfanya aingie kwenye ulevi na hali hiyo imetokana na uamuzi wake wa kuomba kupandishwa daraja na ndipo ulipoibuka ugomvi kati yake na viongozi.
Swai aliongeza kuwa anashangazwa na kusimamishwa kufundisha huku akitakiwa kuripoti shuleni na kutia saini kila siku na kuchukua mshahara kila mwezi.
Alisema tangu mwaka 2013 alisimamishwa kazi na mshahara wake anachukua kama kawaida ila hakuna hatua nyingine za kinidhamu zinazoendelea dhidi yake.
Mratibu wa Elimu Kata, Nuru Faraji, alisema ni kweli mwalimu huyo amekuwa na tabia ya kulewa muda wa kazi na alishawahi kufanya hivyo hata kwenye kikao kimoja na viongozi wa elimu wa wilaya, hali ambayo ilibidi kutolewa kwenye kikao na kupewa adhabu.
Naye Ofisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Selemani Mtinda, alisema wanafahamu tatizo la mwalimu huyo na kueleza kuwa kesi yake iko mamlaka inayoshuhulika na walimu, ambayo ndiyo yenye mamlaka na jambo hilo.
Post a Comment
karibu kwa maoni