Chama cha Skauti Tanzania kinatarajia kuadhimisha miaka Mia
Moja ifikapo Tarehe 21 hadi 28 Julai Mwaka huu katika Kampasi ya Chuo
Kikuu Makao Makuu Mjini Dodoma kwa kushirikisha Vijana wapatao 5,000
kutoka Wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na zaidi ya
wageni 1,000 kutoka Nje ya Tanzania.
Mkuu wa Skauti Tanzania Bibi Mwatum Mahisa alieleza hayo akiuongoza
Ujumbe wa Viongozi Tisa wa Chama hicho Bara na Zanzibar alipokuwa
akitoa Taarifa hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bibi Mwatum alisema vugu vugu la maadhimisho hayo limekuja kufuatia
ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Nne Mh. Mizengo
Piter Pinda alipofanya ziara ya kuhudhuria maadhimisho ya Skauti Nchini
Uganda Mwaka 2016 na kushawishika na Maadhimisho hayo.
Alisema kutokana na uzito wa maadhimisho hayo Kitaifa
yatakayoambatana na maonyesho na mambo mbali mbali Tuzo maalum
zitatolewa kwa Marais waliopita pamoja na watu waliofanya ushujaa zaidi
katika utekelezaji wa ujenzi wa Taifa kiuzalendo.
Mkuu huyo wa Skauti Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba mipango imeanza kuchukuliwa katika hatua za awali za
maadhimisho hayo ambapo Vijana Kumi wa Skuli za Msingi na Kumi
Sekondari wataandaliwa kila Halmashauri za Wilaya Nchini washiriki
kwenye tukio hilo muhimu.
Alieleza kwamba Wizara za Elimu, Afya, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje,
Tamisemi pamoja na ile inayosimamia Utamaduni kwa upande wa Tanzania
Bara zimeshateuliwa na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa kusimamia
jambo hilo la Kihistoria.
Bibi Mwatum alifahamisha kwamba Mataifa Manne ya Kigeni ambayo ni
Korea, Poland, Uganda, na Malawi yameshathibitisha kuhudhuria
Maadhimisho hayo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina
pingamizi kwa Vijana wake katika kushiriki Maadhimisho hayo ya Miaka 100
ya Skauti Tanzania.
Balozi Seif alisema Skauti ni sehemu muhimu na adhimu kwa kuwaandaa
Vijana katika muekeo wa kuwa na Utii, Heshima na Maadili mema, lakini
kubwa zaidi ni kujengeka katika mazingira ya kuwa Wazalendo kwa Taifa
lao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Viongozi
wa Skauti Tanzania kwamba anaiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar kutekeleza wajibu wa kulishughulikia suala hilo katika
kuwaanda Vijana wa Zanzibar wawe sehemu ya maadhimisho hayo Kitaifa.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi huo wa Skauti Tanzania kwa utayari
wao wa kuhakikisha lengo la kuanzishwa kwa Chombo hicho muhimu Nchini
Tanzania linafanikiwa.
Chama cha Skauti ndani ya Ardhi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kimeasisiwa Visiwani Zanzibar mnamo Mwaka 1912.
Post a Comment
karibu kwa maoni