0
Karibu katika mtandao wetu, ujifunze nasi ili uweze kuboresha maisha yako. Naamini kama umekuwa mfuatiliaji wa makala zetu na umekuwa unayafanyia kazi yote ambayo tunajifunza katika mtandao huu, hakuna wakukuzuia kufikia kule unakotarajia, kwa sababu haya yote ambayo unajifunza yameshafanya kazi kubwa katika maisha yangu, hivyo bila shaka na kwako pia yatafanya. Haya si mambo ya kubuni tu, bali ni mambo halisi yenye uwezo wa kukutengenezea matokeo chanya.
Rafiki yangu, awali ya yote, napenda ufahamu kuwa shida, taabu, magonjwa, maangaiko, umaskini na hali zozote ambazo si nzuri katika maisha yako, husababishwa na watu. Ukijaribu kuchambua katika kila changamoto unayopitia katika maisha, utagundua nyuma yake kuna mtu ambaye alizisababisha. Yawezekana ni ndugu, mke, mume, mchumba, rafiki au jamaa. Kwa hiyo watu wanaokuzunguka wanaathari kubwa sana katika maisha. Athari zao katika maisha yako zaweza kuwa chanya au hasi.
Ukichunguza vyema maisha yako lazima utaona yupo aliyehusika kukufikisha katika changamoto uliyonayo. Lakini habari njema ni kuwa, uchaguzi wa kuamua kuendelea kuwa kwenye maisha ya changamoto au kuelekea kwenye mafanikio ambayo unayatamani, u-mikononi mwako. Wewe ndiye unayeweza kuamua. Kama umechoshwa na maisha ya changamoto na uchungu mkubwa huna budi kuamua sasa kuwa mbali na baadhi ya watu; watu ambao wamekufikisha katika hali uliyonayo sasa.
Ndugu yangu, wapo watu ambao wamebobea katika kuua maono ya wenzao. Watu hawa ni marafiki zako, ambao pengine bila kujua athari zao katika maisha, unaambatana nao. Wanaendele kuua maono yako, kuua kujiamini kwako, wanakuwekea giza mbele yako hadi unafika mahali unakubali kuwa wewe ni wa chini kama wao. Yaani kazi yao katika maisha ya wengine ni kuwavunja moyo, kuwafanya wezao wasisonge mbele kimafanikio. 
Na wao katika maisha yao wamejaa shida na changamoto zakutosha. Kwa hiyo wanachofanya ni kutafuta washirika watakao endana nao kwa hali zao za maisha. Wanafanya hivyo ili kuhalalisha uvivu na uzembe wao. Watauwa kila kitu kizuri ambacho chataka kuchomoza ndani yako. Wamejaa sumu. Watu hawa kazi yao kubwa ni kugawa na kufitinisha. Watawagawa kama mpo kundi, au kama upo pekee yako watakugawa katika maono yako, na mwishowe utashindwa kuamini kile ulichonacho. 
Watu hao ndiyo ambao wamekuwa wakikuzuia kusogea mbele katika mafanikio. 

Ulianza kuchua hatua vizuri ya kufanikisha ndoto zako lakini ulisahau kuondokana na watu hawa ambao ndiyo waliokufikisha hapo ulipo. Pengine waweza niuliza kivipi? Kupitia mazungumzo, matendo na tabia zao, vyote hivyo vinakuathiri wewe, bila hata ya wewe kuona kwa haraka, labda utafakari vya kutosha. 
Paulo katika waraka wake kwa Warumi 16:17 anasema “Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza......; mkajiepushe nao.” Hapa Paulo anataka uwaangalie, yaani uwatambue kisha ujiepushe nao. Wafanyao fitina ni wale ambao wanakugawa au kukutenga na watu ambao ni muhimu katika maisha yako, au kukutenga na kile ambacho ulikiamini katika maisha ya kesho yako na ukaanza kukitendea kazi.
  
Watu hao wanakufitinisha na maono au ndoto zako, wanakufanya usione tumaini la kesho yako. Wanakufanya Upoe, ujione kama wao, ujione wa kawaida sana. Ukikaa nao utajiona usiye na hamasa tena. Rafiki yangu, madamu umeamua kuanza safari mpya ya mafanikio, nakusihi, waangalie yaani watambue na uwaepuke kabisa. Acha kutaniana nao, acha kuongea nao kama hakuna cha muhimu, acha kukaa nao kama ikibidi. Anza kutafuta jamii mpya, jamii ya wenye mtizamo na maono kama yako ili uweze kuvutia mema upande wako.Kumbuka kadiri utakavyomtambua mmoja wa watu hao na ukajitenga naye hakika utaanza kuons mabadiliko ya mustakabali wa maisha yako. 
Asante kwa kuongozana nami toka mwanzo hadi tamati; endelea kujifunza kupitia mtandao huu kila siku bila kusahau kuwaalika na wengine kujifunza nasi. Jiunge na mtandao wetu mpya wa Alex Mushi dot Com, ambao ni mahsusi kwa ajili ya kukulea ili uweze kufikia ndoto zako katika maisha; Maana mafanikio makubwa unayotaka kuyafikia huwa rahisi pale unapopata mtu wa kukuongoza njia ya kupita. Kwa hiyo mtandao huo mpya ni maalumu kwa kazi hiyo, kujua utaratibu wa kujiunga,
Alex Mushi,
Mwalimu na Mwandishi,
Dodoma-Tanzania. 
Simu:     075 6 364 075/062 5 653 239

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top