0

Jeshi la Polisi limesema hali sasa ni shwari kwa kuwa vitendo vya unyang’anyi vimepungua, lakini likasema hali ya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo ni mbaya.

Jeshi hilo pia limesema limefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa mauaji yanayofanywa na watu wasiojulikana katika wilaya tatu za mkoani Pwani.

“Tatizo kubwa kwa sasa ni ubakaji na ulawiti. Hii inatokana na makosa mengi sasa yanaripotiwa kwa sababu ya ufahamu wa wananchi kuongezeka,” alisema msemaji huyo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi (ACP), Barnabas Mwakalukwa alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited zilizopo jijini Dar es Salaam jana.

Mwakalukwa, ambaye alikuwa katika ziara yake ya kwanza kwenye vyombo vya habari tangu ateuliwa kushika nafasi hiyo alisema kwa sasa nchi ina amani na utulivu kwa kuwa vitendo vya unyang’anyi wa kutumia silaha, uporaji, mauaji ya vikongwe na albino yamepungua.

Mwakalukwa, ambaye pia ni mchambuzi wa uhalifu, alisema vitendo vya ubakaji na ulawiti vinakua kwa kuwa sasa wananchi wengi wamesahau maadili yao kama Watanzania.

Alisema kwa sasa mitandao ya kijamii imeathiri jamii, lakini pia watu hawana maadili tena kiasi kwamba wanaona  hawana wajibu wa kuwaelekeza watoto wa wenzao.

“Hata wazazi nao wamesahau majukumu yao ya malezi, lakini pia tunaaminiana kupita kiasi. Mgeni anakuja nyumbani kwako, unaruhusu alale na watoto bila kujua athari wanazoweza kuzipata,” alisema.

“Mgeni anamnajisi mtoto lakini kwa sababu ni mtu wa karibu na familia taarifa hazifiki kituoni. Kunakuwa na mgogoro katika familia. Mama analalamika sana, lakini baba anataka wayamalize katika level (ngazi) ya familia. Matokeo yake taarifa zinaletwa zikiwa zimechelewa sana.”

Mwakalukwa, ambaye hakutoa takwimu za kukua kwa vitendo hivyo, alisema kesi nyingine za ubakaji zinatokana na wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili.

 “Wanakutana na mteja, lakini wasipokubaliana, wanafanyiwa vitendo vya unyanyasaji na wanakuja kuripoti polisi kwamba wamebakwa,” alisema kamanda huyo.

Kuhusu wizi, Mwakalukwa ambaye amechukua nafasi ya Advera Bulimba aliyehamia Mwanza, alisema umepungua mitaani kutokana jeshi hilo  kushirikina na wadau kutoa elimu na kuhamasisha.

“Mabenki sasa yamewaelimisha wateja wao kutotembea na fedha nyingi, lakini pia watu hawakai na fedha nyingi nyumbani hivyo hata wahalifu wanaona wakivamia hawawezi kupata kitu,” alisema.

Alisema suala jingine lililopunguza uhalifu ni kupiga marufuku pikipiki za abiria, maarufu kama bodaboda kuingia mijini.

Alisema bodaboda zilikuwa zinatumiwa na wahalifu na kwamba waathirika wakubwa wa vitendo hivyo walikuwa wanawake kutokana na kupenda kutumia usafiri huo.

Alisema wengi waliporwa mikoba yao, fedha na hata kubakwa.

“Unajua wakati tunasema pikipiki zisiingie mjini, watu hawakutuelewa lakini niwaambie tu uamuzi ule umeleta mafanikio sana. Wanawake walikuwa waathirika wakubwa wa matukio ya uvamizi, walikuwa wakiibiwa mikoba yao na kunyang’anywa vitu vya thamani lakini sasa hali ni tofauti,” alisema.

Hata hivyo, Mwakalukwa ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa msemaji wa jeshi hilo alikuwa kitengo cha operesheni mkoani Mwanza, alisema pamoja na uhalifu kupungua mitaani, wahalifu wamebuni mbinu mpya; sasa wanaiba kwa njia ya mitandao.

Kazi kubwa

“Kwa sasa  kuna kazi kubwa ya kumaliza uhalifu wa njia ya mtandao kwa sababu baada ya teknolojia kupanuka, wahalifu hawatumii tena silaha na badala yake wanaiba kwa njia ya mtandao,” alisema.

“Unajua wengi wanatapeliwa na kuibiwa ila hawasemi, wananchi wanafikiri wanasiasa ndiyo waathirika wakuu. Ngoja nikwambie hao ni idadi ndogo sana ukilinganisha na wananchi wa kawaida.

“Sasa wahalifu wanakuja moja kwa moja kwenye wallet (pochi) yako kupitia ATM. Wanachofanya ni kutumia mitandao. Hivyo kazi bado kubwa na kinachotakiwa zaidi ni kutoa elimu ili watu wasihamishe fedha kwa mtu aliyemtumia tu ujumbe mfupi wa simu kwamba atume fedha,” alisema.

Sirro anastahili sifa

Mwakalukwa pia alizungumzia mauaji yanayoendelea katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga akisema hali sasa ni shwari na kumsifu mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kwamba amefanya kazi kubwa.

“Kibiti sasa kuna amani. Kibiti itabadilika kwani hata sasa  hatusikii tulivyokuwa tukiyasikia. Waandishi tusifanye propaganda kuwa Kibiti haikaliki. Hali sasa shwari na sisi tumeanzisha mkoa maalumu wa kipolisi, maana yake usalama sasa upo,” alisema Mwakalukwa.

Alisema kwa jinsi hali inavyoendelea, itafikia wakati Kibiti itakuwa sehemu nzuri ya kuwekeza tofauti na watu wanavyosema sasa kuwa ekari kumi inauzwa Sh1,000 kuonyesha kuwa wilaya hiyo si salama .

“Ninachowashauri ni kwamba andikeni habari nzuri za Kibiti,” alisema.

Wilaya hizo tatu zimekuwa zikibaliwa na mauaji ya viongozi na watendaji wa vijiji na vitongoji tangu Mei mwaka jana.

Katika matukio machache, wauaji hao waliacha ujumbe kuwa viongozi hao wamekuwa wakidhulumiwa na watendaji wa Serikali, lakini mauaji hayo ya visasi yamekuwa yakitia shaka kutokana na matumizi ya silaha na kulenga polisi pia.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top