HADI sasa haijagunduliwa teknolojia ya kuaminika, inayoweza kutabiri kutokea kwa matetemeko ya ardhi popote Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla. Akizungumza mwishoni mwa wiki ofisini kwake mjini Dodoma, Mjiolojia Mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Gabriel Mbogoni alisema teknolojia hiyo haipo popote duniani.
“Teknolojia ya kutabiri kutokea kwa matetemeko ya ardhi haijagunduliwa bado hata kwenye nchi zilizoendelea, hivyo tujue kwamba tetemeko halibishi hodi na halina taarifa,” alisema Mbogoni.
Mbogoni, Mjiolojia aliyebobea katika masuala ya matetemeko, alisema vifaa vilivyopo duniani kote, vinapima ukubwa wake kwa kipimo cha Richter ambacho ni kati ya 0 hadi 10 na tabia ya tetemeko ambayo kwa kawaida hayana mipaka ya kijiografia.
Alisema Tanzania kama nchi nyingine za Afrika Mashariki zimekumbwa na matetemeko kama lile lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka jana majira ya saa 9.27 alasiri, ambalo lilikuwa na ukubwa wa 5.7 wa kipimo cha Richter.
Tetemeko hilo liligusa pia sehemu ya Kusini ya Uganda na lilianzia umbali wa kilometa 10 chini ya ardhi. Mbogoni alisema licha ya tetemeko kutopiga hodi, lakini kuna baadhi ya wanyama wa kufuga kama ng’ombe, mbuzi, kuku na pengine panya, wanaweza kuonesha ishara ya kutokea kabla ya kutokea kwake.
Alisema kitu cha ajabu ishara hizo kwa wanyama hao, huonekana kwa muda mfupi wa sekunde chache kabla ya tukio lenyewe. Hivyo kama mtu anaweza kugundua tofauti ya wanyama wanatabiri matukio na wakati kusipokuwa na matukio, inaweza kumsaidia binadamu kujihadhari.
Alisema matetemeko yanatokea kila mahali, lakini nchi zilizomo kwenye Bonde la Ufa kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini, zipo kwenye hali tete zaidi, kwani eneo hilo huwa na fukuto kali la joto kutokana na ukweli kwamba tabaka la miamba migumu kwenye maeneo hayo huwa na kina kifupi.
Hivyo,Tanzania ipo kwenye hali tete ya kupatwa na tetemeko la ardhi kutokana na kupitiwa na mikondo miwili ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, ambapo mmoja unapita Mashariki ya Nchi na mwingine Magharibi.
Alisema mkondo wa Mashariki wa Bonde la Ufa, unapita katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Dodoma hadi Iringa wakati ule wa Magharibi unapita katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa, Katavi, Mbeya, Njombe na Ruvuma.
“Maeneo ambayo hayapo kwenye Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, kina cha tabaka la miamba migumu huwa ni kati ya kilometa 35 hadi 40 wakati maeneo yaliyopo kwenye bonde hilo, kina cha tabaka la miamba migumu huwa hadi kilometa 10,” alisema Mbogoni.
Alisema maeneo yote mawili, yanapatwa na tetemeko la ardhi, japo yanapishana utete na ugumu wa tabaka la miamba, kwani sababu zinazofanya litokee ni zilezile za kuwapo kwa fukuto kati ya dunia.
Mbogoni alisema maeneo yenye kina kifupi cha miamba migumu, huwa rahisi zaidi kuathiriwa na nguvu za asili za mgandamizo na fukuto la joto kali kutoka kwenye tabaka la kati la dunia kuliko kuwa na kina kirefu za miamba migumu.
Alisema licha ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika kuwa na hali tete kutokana na kupitwa na Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, pia maeneo mengine yaliyo nje ya bonde hilo hayapo salama.
Alieleza kuwa matetemeko hayana mipaka ya kijiografia na alitoa mfano wa tetemeko lililotokea Karonga nchini Malawi Desemba 27, 2009, kwamba lilisambaa umbali wa kilometa 150 hadi mkoani Mbeya Tanzania na lilikuwa na ukubwa wa 5.9 katika Richter
Post a Comment
karibu kwa maoni