0
UONGOZI wa wafanyabiashara wa Tanzania bara na Zanzibar wametoa siku 30 Rais John Magufuli kuhakikisha anatatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao vinginevyo maduka yote hata ya vichochoroni yatafungwa, anaandika Dany Tibason.
Kauli hiyo nzito imetolewa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja wakati akihitimisha kikao cha siku mbili cha halmashauri kuu ya jumuiya hiyo.
Minja akisoma maazimio hayo sita yaliyofikiwa katika vikao hicho alisema, lengo kubwa ni kuhakikisha changamoto za wafanyabiashara zinatatuliwa.
Katika maazimio hayo pamoja na kutaka changamoto zitatuliwe wamesema kuwa hawataki kero zao zitatuliwe na kiongozi yoyote isipokuwa rais wa nchi ambaye ni Dk.John Magufuli.
“Halmashauri kuu taifa imeagizwa kumuona mheshimiwa rais kuzungumzia mwenendo mzima wa ufanyaji biashara wa wamachinga kutaka ushuru wa huduma (service levy) iondolewe kwenye maduka badala yake ibakie kwenye makampuni na maduka makubwa,” amesema Minja.
Ametaja maazimio mengine ni pamoja na kuitaka taasisi ya rais, kufuta agizo la waziri wa fedha kwamba mashine ya EFD ikiharibika ndani ya saa 48 na mfanyabiashara akiwa na uthibitisho wa barua kutoka Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), akamatwe na alipe faini.
Pia imeazimiwa kuwa tangazo la TRA kuhusu kubadili mashine za EFD lirekebishwe, badala ya kutaka wafanyabiashara kununua kwa mara ya pili mashine hizo mawakala ndiyo watakiwe kubadilisha mashine husika.
Aidha, wametaka wafanyabiashara ambao wameishalipa gharama za kupatiwa mashine na hawajapatiw, wapatiwe mashine zao mara moja.
Minja amesema utitiri wa tozo mbalimbali za halmashauri na taasisi nyingine ziainishwe ili ambazo ni kero zifutwe kama rasi alivyoagiza huku zenye mashiko ziunganishwe na kuwekwa kwenye malipo ya leseni.
Amesema wameazimia kukabiliana na kaasumba inayoendelea ya kufunga maduka bila kuwa na uthibitisho wa maamuzi ya kimahakama.
“Kutokana na maazimio haya tunawaagiza wafanyabiashara wote nchini kuendelea kutoa huduma kama kawaida ndani ya mwezi mmoja wakati bodi ya uongozi ikitekeleza maagizo na maazimio ya halmashauri kuu baada ya muda huo bodi itatoa mrejesho juu ya hoja hizi,” ameeleza Minja.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top