0

Ni jambo la nadra kwa wananchi kuwagomea viongozi wa juu wa Serikali, hususan wanapokutana nao ana kwa ana, lakini Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amegomewa na kulazimika kuunda kamati kuchunguza madai yao.
Mara nyingi, wananchi wanapokuwa na madai yao huomba yatatuliwe, lakini ni nadra kuwakatalia viongozi wakisisitiza kupatiwa haki wanazotaka.
Hata hivyo, wananchi wa Kitongoji cha Saitabau kilichopo katika Kata ya Tarakwa wilayani Arumeru wamegoma kujiunga na Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni na kuruhusu mradi wa maji katika kijiji chao kuwa chini ya mamlaka hiyo.
Kutokana na mgomo huo, Gambo ameamua kuunda kamati ya wataalam kutoka ofisini kwake ili kuchunguza mgogoro huo.
Wakizungumza na Gambo aliyefika katika kitongoji hicho, wananchi hao walisema hawataki kujiunga na mamlaka hiyo kwa kuwa hawajui faida zake, badala yake wanachoona ni kunyang’anywa mradi wa maji.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Lucas Lukumai alisema wananchi wanapinga kujiunga na mamlaka hiyo kutokana na kutopatiwa elimu.
Pia, alisema wanapinga kuhamishwa kwa madai kwamba mamlaka hiyo inataka kuchukua mradi wao wa maji ambao waliuchangia na kusaidiwa na shirika la misaada la kimataifa la Oxfam.
“Mimi nilikamatwa na kuwekwa rumande na polisi kwa agizo la mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kwa tuhuma za kuikataa mamlaka jambo ambalo si kweli. Wanaokataa ni wananchi wenyewe kwani hawajapewa elimu,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni walipewa fursa ya kukutana na wananchi hao ili kuwapa elimu, lakini wameshindwa kufanya hivyo na badala yake wanawatuhumu viongozi kuwa nyuma ya mgomo wa wale wanaowaongoza.
Akijibu tuhuma hizo, Mtendaji Mkuu wa mamlaka ya mji huo, Sophia Shoko alisema wananchi wanagoma kujiunga na mamlaka kwa kuwa hawataki mradi wao wa maji uwe chini ya Ngaramtoni.
“Hapa kuna mradi wa maji, wenyewe hawataki uwe chini ya mamlaka ili maji yasambazwe maeneo mengine na wanataka kuendelea na malipo ya Sh500 kwa mwezi jambo ambalo si sahihi,” alisema.
Hata hivyo, Diwani wa kata hiyo, Elihuruma Laizer alimuomba mkuu wa mkoa kuunda kamati maalumu ya kuchunguza suala hilo na kutafuta nafasi ya kukaa na wananchi kuwasikiliza kwa kuwa jambo hilo lina mgogoro alioutaja kuwa ni mkubwa.
Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Gambo alikubaliana na ushauri wa diwani wa kata hiyo kuunda kamati maalumu ya kuchunguza mgogoro huo kabla ya kuchukua hatua stahiki.
“Nitaunda kamati ya wataalamu kutoka ofisini kwangu, watakuja hapa na kuzungumza na wananchi, viongozi wa mamlaka ya mji mdogo na viongozi wa kitongoji na baadaye watanipa ushauri kufikia uamuzi,” alisema.
Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni iliundwa mwaka 2016 na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ili kupeleka huduma za kiserikali karibu zaidi na wananchi, lakini ilikutana na kigingi hicho cha wananchi wanaotaka waachwe waendelee kuwa nje ya utawala wake.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top