Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya
ya bidhaa za mafuta ya petroli nchini, ambapo kuanzia leo bei za
rejareja za bidhaa hizo zimepanda kwa Sh 10 kwa lita, ikilinganishwa na
bei iliyopita huku bei ya mafuta ya taa ikishuka.
Kwa
mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Godwin Samwel, kuanzia
Septemba mwaka huu, bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka
kwa Sh 10 kwa lita sawa na ongezeko la asilimia 0.53 na Sh 57 kwa lita
sawa na asilimia 3.10.
Hata hivyo, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa Sh 19 kwa lita sawa na asilimia 1.04.
Aidha,
ilisema kuwa kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla
za petroli na dizeli, nazo zimeongezeka kwa Sh 10.41 kwa lita sawa na
asilimia 0.56 na Sh 56.74 kwa lita sawa na asilimia 3.30.
Alisema kwa upande wa mafuta ya taa, bei ya bidhaa hiyo imepungua kwa Sh 10.01 kwa lita sawa na asilimia 1.11.
Alifafanua
kuwa ongezeko la bei za petroli na dizeli kwenye soko la ndani,
limetokana na ongezeko la bei za mafuta hayo katika soko la dunia na
ongezeko la gharama za usafirishaji wa mafuta hayo (BPS premiums).
Kupungua
kwa bei ya mafuta ya taa kunatokana na kupungua kwa gharama za
usafirishaji wa mafuta hayo, ijapokuwa bei ya mafuta hayo imeongezeka
katika soko la dunia.
Alieleza
kuwa kutokana na mabadiliko hayo mapya ya bei za bidhaa za mafuta, bei
za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote katika mkoa wa Tanga, nazo
zimebadilika, ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe Agosti 2,
mwaka huu.
Katika
mkoa huo, kuanzia Septemba mwaka huu, bei za rejareja za petroli
zimeshuka kwa Sh 13 kwa lita sawa na asilimia 0.65 wakati bei za Dizeli
na Mafuta ya Taa zimeongezeka kwa Sh 14 kwa lita sawa na asilimia 0.78
na Sh 106 kwa lita sawa na asilimia 6.21.
Aidha,
bei za jumla za petroli zimeshuka kwa Sh12.98 kwa lita sawa na asilimia
0.69 wakati bei za dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa Sh 14.47
kwa lita sawa na asilimia 0.83 na Sh 105.88 kwa lita sawa na asilimia
6.65).
Samwel
alifafanua kuwa kupanda na kushuka kwa bei za mafuta mkoani Tanga,
kunatokana na mabadiliko ya bei za mafuta hayo katika soko la dunia na
ongezeko la gharama za usafirishaji wa mafuta hayo.
Alisema
vituo vyote vya mafuta, vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta
katika mabango, yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta.
Post a Comment
karibu kwa maoni