MTOTO wa
miaka saba aliyelelewa kama mtoto wa kike kutokana na maumbile yake kutoeleweka
vema, baada ya vipimo vyote katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
ameonekana kuwa ni mwanamume, hivyo amefanyiwa upasuaji wa kwanza wa kushusha
kokwa (mbegu za kiume) kwenda kwenye korodani ili kumrejesha katika hali ya
kawaida.
Daktari
Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Zaitun Bokhary alisema hayo alipofanya
mahojiano maalumu na HabariLeo kuhusu kambi ya wiki moja iliyowekwa kwa ajili
ya kufanya upasuaji ambao ni mgumu, wakishirikiana na wataalamu watano kutoka
Chuo Kikuu cha Oxford nchini Marekani.
Dk Bokhary
alisema upasuaji huo ni hatua ya kwanza katika kumrejesha mtoto huyo katika
hali ya kawaida, hatua nyingine za upasuaji zitafuata, kwani atafanyiwa
upasuaji kwa hatua tatu.
Alisema kwa
kuwa mtoto huyo vipimo vimeshaonesha kuwa ni wa kiume, wametoa ushauri kwa
wazazi wake hususan baba yake kuwa karibu na mtoto huyo ili kumfanya asijisikie
vibaya, kwani awali alikuwa akijisaidia haja ndogo kama mtoto wa kike, pia
alikuwa amepewa jina la kike ikiwa ni pamoja na kuvaa nguo za kike.
“Tumemshauri
baba yake kutembea mara kwa mara na mtoto wake, pia kwenda naye katika michezo
ya kiume, ikiwa ni pamoja na kuanza kumvalisha mavazi ya kiume. “Mtoto huyu
alipoanza kuvaa nguo za kiume kwa mara ya kwanza alikuwa akijisikia aibu kwa
kuwa alishazoezwa mambo ya kike, lakini tunaendelea kutoa ushauri kwa wazazi
ili wawe karibu na mtoto wao asijisikie tofauti yoyote,” alisema daktari huyo.
Aliongeza
kuwa kwa kuwa tayari mtoto huyo alikuwa akisoma katika shule ya msingi mojawapo
jijini Dar es Salaam, hospitali hiyo inafanya utaratibu kupitia kwa daktari
wake ili kuandika barua kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita),
atambuliwe kama mwanamume, ikiwa ni pamoja na kuhamishwa shule aliyokuwa
akisoma.
Alisema kuwa
na sasa mtoto huyo, amehamishwa nyumbani kwao anakaa na ndugu zake eneo lingine
ili aanze kuzoea mazingira mapya ya maumbile yake. Pia Dk Zaitun alielezea
upasuaji mwingine mgumu uliofanyika ni wa mtoto wa siku mbili ambaye alikuwa na
tatizo katika mfumo wa nyongo, njia ilikuwa imefungwa ilibidi apasuliwe
kufungua njia ili mfumo wa nyongo uendelee kama kawaida.
Daktari
bingwa huyo wa upasuaji wa watoto, alieleza upasuaji mwingine walioufanya ni
kwa mtoto aliyekuwa na saratani ya figo zote mbili, moja ilitolewa na nyingine
ilikuwa haijalika ikaondolewa sehemu ya tatizo bila kuathiri mfumo wa misuli.
Alisema
upasuaji wote huo umekwenda vizuri, hali za watoto hao zinaendelea vema.
Alisema kambi ya upasuaji huo ilikuwa Novemba 27 hadi Desemba Mosi, mwaka huu
iliongozwa na Daktari Bingwa Mshauri Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto, Profesa
Kokila Lakhoo kutoka Chuo Kikuu hicho cha Oxford.
Alisema Dk Lakhoo amekuwa
akija hospitalini hapo kila mwaka, kusaidia ule upasuaji ambao ni mgumu, na huu
ni mwaka wake wa tano kufika nchini.
Post a Comment
karibu kwa maoni