0

 
Imeelezwa kuwa majangili 1,063 wamekamatwa katika Hifadhi ya Tarangire kuanzi mwaka 2012/13 hadi kufikia Desemba mwaka jana.

Kati ya hao, 105 walikuwa katika mtandao wa ujangili wa tembo.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho alitoa taarifa hiyo jana kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyotembelea hifadhini hapo.

Batiho alisema askari wa hifadhi hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali na wadau wa utalii, wamefanikiwa kupunguza matukio ya ujangili kutoka matukio 254 mwaka 2014/15 hadi kufikia matukio 67 mwaka jana.

Alisema mwaka 2012/13 kulikuwa na matukio 179 ya ujangili, mwaka 2013/14 (180), 2014/15 (254), 2015/16 (126) na mwaka 2016/17 matukio 257.

Hata hivyo, Batiho alisema licha ya kukabiliana na matukio ya ujangili, mapato ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo yameongezeka kutoka Sh9.7 bilioni mwaka 2012/13 hadi kufikia Sh19 bilioni mwaka 2016/17.

Alisema ongezeko hilo la mapato limetokana na idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje.

Batiho alisema watalii wa nje wameongezeka kutoka 112,163 mwaka 2012/13 hadi kufikia watalii 140,405 mwaka 2016/17.

“Watalii wa ndani pia wameongezeka kutoka 65,038 mwaka 2012/13 hadi kufikia watalii 76,022 mwaka 2016/17 na idadi inaongezeka zaidi,” alisema Batiho.

Wakizungumzia taarifa hiyo, wabunge wa kamati hiyo, waliipongeza hifadhi hiyo kwa jitihada za kupambana na ujangili na kuongeza mapato yake.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Risala Kabongo alisema mafanikio ambayo yapo sasa Tarangire ni makubwa.

Alishauri uongozi wa hifadhi hiyo kuendelea kuboresha miradi ya ujirani mwema ili jamii ishiriki katika vita dhidi ya ujangili na uhifadhi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kamilembe Luota alisema Hifadhi ya Tarangire imefanya kazi nzuri katika kupambana na majangili na kuongeza watalii.

Awali katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema kwamba wizara hiyo imepokea ushauri wote uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo na utafanyiwa kazi ili kuhakikisha watalii wanaongezeka nchini sambamba na kulinda rasilimali.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top