0
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amewataka wakazi mkoani hapa kudai risiti baada ya kufanya manunuzi ili kuepuka mkono wa dola.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Gambo alisema, mtu atakayekamatwa na vitu bila kuwa na risiti atapigwa faini ya Sh. 75,000 hadi Sh. milioni 1.5.

Alisema faini hiyo itawahusu wafanyabiashara wanaouza bila kutoa risiti, wanunuzi na hata madereva wanaopakiza abiria wao na bidhaa bila risiti.

"Tunafanya hivi sababu serikali tunapoteza fedha nyingi kwa sababu ya wafanyabiashara hawatoi risiti na wanunuzi hawadai risiti," alisema.

Alisema kutoa risiti kunachangia kupandisha makusanyo ya mkoa na kwa mwaka 2016/2017, mkoa ulikadiria kukusanya Sh. bilioni 28, lakini hadi kufika katikati ya Desemba, walikusanya Sh. bilioni 27 hali inaonyesha lengo litapita hadi kufika mwaka wa fedha unaofuata.

"Hali hii inatokana na watu kutoelewa dhana ya kudai risiti na kutoa japo bado wafanyabiashara na wanunuzi wengi hawazingatii maelekezo hayo na kusababisha upotevu wa fedha za serikali.

“Ni vema kila mtu akaelewa ana jukumu la kusaidia makusanyo, serikali yake kwa ajili ya kuharakisha maendeleo,” alisema.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top