0
SERIKALI imesema, hali ya uchumi wa nchi inaendelea kuwa imara kwa kiasi cha kuridhisha taasisi mbalimbali za kimataifa. Kwa mwaka huu wa fedha, unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika.
Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi.
"Ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani zimetabiri kuwa wakati uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia 3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 katika mwaka 2018," alisema.
Aidha alisema moja ya ajenda kuu za Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi mpya wa viwanda, ambapo hadi kufikia mwaka jana viwanda 3,300 vilisajiliwa, Ujenzi na uzalisha katika viwanda hivi uko katika hatua mbalimbali.
Alisema kati ya miradi hiyo iliyosajiliwa, viwanda vikubwa ni 652 na viwanda hivyo vyote vina jumla ya mtaji wa zaidi ya Sh trilioni tano, utakaowekezwa nchini na vitaajiri watu 50,625 ambapo mwezi ujao Alisema, katika sekta ya nishati, Serikali inaendelea kutekeleza miradi 20 ya kuhakikisha nchi ina umeme wa uhakika na miongoni mwa miradi ya kimageuzi ni usimikaji wa mitambo ya umeme wa gesi Kinyerezi I (mtambo wa nyongeza wa megawati 185) na Kinyerezi II wa Megawati 240 ambayo kwa pamoja itaongeza megawati 425.
Alisema mtambo wa Kinyerezi I- Nyongeza umefikia asilimia 50 na mtambo wa Kinyerezi II umekamilika kwa asilimia 87, ambapo Desemba mwaka jana mtambo huo wa kisasa umeingiza megawati 55.94 katika Gridi ya Taifa na kiasi kingine cha megawati 27.94 kinatarajiwa kuingia kwenye gridi mwezi huu.
Aidha alisema, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kwa kuanzia na kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kitakachogharimu Sh Trilioni 2.7.
"Kazi ya kusanifu njia yote itakayopita reli imeshakamilika na kwa sasa uandaaji wa tuta, ujenzi wa madaraja kabla ya kutandika reli umeanza kwa kasi na watu wanafanya kazi usiku na mchana...Tanzania ya miaka miwili ijayo itakuwa tofauti sana," alisema.
Alisema ujenzi wa kipande cha pili cha kilomita 442 (Morogoro- Makutupora- Dodoma), kitakachogharimu Sh trilioni 4.3 mkandarasi wake ameshaanza maandalizi. Pia alisema wakati ujenzi wa reli ukiendelea, Serikali kupitia kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (RAHCO) imeshatangaza zabuni kwa ajili ya kupata makampuni yatakayotengeneza vichwa na mabehewa ya kisasa ya treni ya umeme na mafuta na zabuni zitafunguliwa mwezi huu.
Alisema katika zabuni hiyo, Serikali inatarajia kununua vichwa 25 (23 vya umeme na viwili vya dizeli), mitambo 25 ya ukarabati wa reli na mabehewa 1,590 (kati ya hayo 1,530 yakiwa ni ya aina mbalimbali za mizigo, mabehewa 60 ya abiria (15 yakiwa ni daraja la kwanza na 45 daraja la kawaida).
Katika hatua nyingine, Dk Abbasi alisema katika Ziwa Nyasa mwishoni mwa wiki iliyopita meli mbili mpya za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma zinazobeba mzigo tani 1,000 kila moja zimeanza safari kwenda bandari mbalimbali zikiwemo nchi za jirani. "Serikali imetumia Sh bilioni 11.252 na meli nyingine mpya ya abiria itakamilika Juni mwaka huu.
Katika Ziwa Victoria, kupitia kampuni ya Serikali ya Huduma za Usafiri katika Maziwa, mkandarasi wa kutengeneza meli mbili kubwa, mpya na za kisasa amneshapatikana," alisema.
Akizungumzia Serikali kuhamia Dodoma alisema, imeendelea kuonyesha nidhamu ya kuahidi na kutekeleza ahadi hiyo ambapo hadi kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka jana, viongozi waandamizi wa Serikali wameshahamia Dodoma na Rais, John Magufuli akiwatarajiwa kuhamia mwaka huu.
“Jumla ya wafanyakazi 3,617 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za umma wameshahamia Dodoma na awamu inayofuata mwaka huu itahusisha wafanyakazi wengine 2,460, “ alisema.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top