Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa wilaya ya Songea mkoani
Ruvuma wajikite kwenye zao la kahawa ili wawe na zao mbadala la
biashara.
Ametoa
wito huo jana Januari 5, 2017 wakati akizungumza na wakazi wa kijiji
cha Lipokela na vijiji jirani, wilayani Songea mara baada ya kukagua
shamba la kahawa la Aviv Tanzania lenye ukubwa wa hekta 1,990.
“Limeni
kahawa ili mpate fedha sababu zao hili ni la biashara. Kahawa ni
miongoni mwa mazao matano ya biashara ambayo Serikali ya awamu ya tano
imeamua kuyawekea mkazo ili yaweze kuongeza tija kwa wakulima na kuinua
uchumi wa Taifa,” alisema Majaliwa.
“Tumeamua
kuweka mkazo kwenye mazao matano ya pamba, kahawa, chai, korosho na
tumbaku kwa sababu yanaleta tija na kuliingizia Taifa fedha za kigeni,”
alisema na kuongeza.
“Tumefanya
tathmini na tumegundua udhaifu mkubwa mkubwa katika usimamizi wa mazao
haya ndani ya Serikali kuanzia ngazi ya Halmashauri.”
Waziri Mkuu alisema ni lazima wananchi walime zao hilo na viongozi wahakikishe wananchi wananufaika na zao hilo.
Hata
hivyo, alionyeshwa kutoridhishwa na utendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Songea baada ya kuelezwa kuwa kampuni ya Aviv Tanzania imezalisha
miche milioni moja lakini iliyochukuliwa na kusambazwa kwa wananchi ni
miche isiyozidi 200,000.
“Kampuni
hii imeamua kutoa miche ya bure kwa wakulima, wamezalisha miche milioni
moja lakini hadi sasa imechukuliwa 200,000 tu. Kuna miche zaidi ya
800,000, imebaki, na tena wawekezaji hawa wanatoa elimu bure ya kulima
na kuitunza mikahawa yako,” alisema.
Amewataka
wakulima hao watenge ekari moja hadi tatu kwa kila kaya ili waweze
kulima zao hilo. “Wana Lipokela tengeni ekari moja hadi tatu za kulima
kahawa, tukifanya hivyo suala la fedha kupitia kahawa litakuwa
limekamilika,” alisema.
Amesema
itabidi zao la kahawa liundiwe mfumo maalum wa ununuzi ambao ni wa
ushirika kwa kuzingatia vyama vya msingi (AMCOS) vilivyokuwepo.
Mapema,
akitoa taarifa juu ya shamba hilo, Meneja wa Aviv Tanzania, Bw. Medu
Medappa alisema lengo la kuanzisha mradi huo lilikuwa ni kuhakikisha
wanapata shamba kubwa la kahawa aina ya Arabica nchini Tanzania lenye
viwango vya kimataifa.
Alisema wamekwishatoa ajira kwa Watanzania wapatao 3,000 zikiwemo za moja kwa moja na za msimu.
Alisema
kampuni hiyo imeweza kuchangia miradi ya maendeleo kwenye vijiji vinne
jirani vya Lipokela, Lusonga, Liganga na Selekano. “Hadi mwaka 2017
tuliweza kukamilisha ujenzi wa zahanatio katika kijiji cha Lipokela,
nyumba ya mwalimu katika vijiji vya Liganga na Lusonga, uchangiaji wa
madawati kwenye vijiji vya Lipokela na Lusonga,” alisema.
Alisema
wameweza kuanzisha scheme ya wakulima wadogo wa nje (outgrowers scheme)
kwa wakulima 2,000 ambao wamegawanyika kwenye vikundi 36 katika vijiji
31 ndani ya mkoa wa Ruvuma.
Waziri
Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea
wilaya ya Mbinga ambako atakagua miche kwenye taasisi ya TACRI,
atatembelea kiwanda cha kukoboa kahawa cha Mbinga (MCCCO), kuzungumza na
watumishi na madiwani na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.
Post a Comment
karibu kwa maoni