0

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT) kupitia chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Bi,Yasmin Bachu amesema ili kuvuka katika chaguzi zijazo lazima wanawake ndani ya jumuiya hiyo kufanya kazi kwa vitendo,uwazi na upendo miongoni mwao.
Kauli hiyo aliitoa wilayani Monduli wakati wa ziara yake iliyolenga kukutana na wanawake kuanzia ngazi ya tawi kwaajili ya kuwashukuru wanawake hao kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti pamoja na kuwapa elimu juu ya masuala ya uongozi ambapo katika ziara hiyo aliambatana na wataalam mbalimbali.
Alisema kuwa ili kuijenga jumuiya hiyo ni wajibu wa wanawake hao kukubali kuvunja makundi ndani na nje ya jumuiya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawarejesha wanachama ndani ya chama hasa wale waliokuwa wakigombea nafasi mbalimbali za chaguzi na kushindwa katika chaguzi hizo.
"Tufanye kazi kwa uaminifu na upendo ndani ya jumuiya kwa kuhakikisha tunawarejesha wenzetu ambao hawakupata nafasi za uongozi katika chaguzi zilizopita,mfanye rafiki na kiongozi mwenzako sababu kila mwanamke ni kiongozi" alisema Bi,Bachu.
Aidha aliwataka wanawake jamii ya kimaasai kuondokana na mila pitofu za ndoa za utotoni na ukeketaji kwakuwa hazina faida katika maisha yao ya baadae.
"Tupende kuhamasishana juu ya umuhimu wa kuachana na mila potofu hasa umuhimu wa kupeleka mtoto shule ndoa za utotoni hazisaidii tuache tamaa ya kupokea ng'ombe kwani kuna faida kubwa ya kupeleka mtoto shule" alisema Mwenyekiti hiyo.
Awali Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Monduli Bi,Ester Wakari alieleza kuwa kama viongozi wana wajibu wa kutoka ofisini na kutembelea  wanachama wao ili kutimiza malengo ya chama tawala pamoja na kujua kero zao wanazokutana nazo.
 Katika ziara hiyo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo masuala ya sheria,uongozi na maendeleo ya ustawi wa jamii.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top