Hayo
yalisemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)
wakati wa majadiliano na wataalamu wa Benki ya Dunia yaliyoongozwa na Makamu wa
Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika Bw. Makhtar Diop,
kwenye mikutano ya mwaka ya kipupwe inayoendelea mjini Washington DC Marekani.
Dkt.
Mpango amesema kuwa miradi ya Kikanda ambayo Benki hiyo imeonesha nia ya kuitekeleza
ni ile ya uboreshaji wa mazingira na bandari katika ziwa Victoria zikiwemo za
mikoa ya Mwanza, Musoma na Kigoma na Bandari zilizoko katika Ziwa Tanganyika
ambazo zitarahisisha usafiri wa kwenda Burundi na Congo.
‘Miradi
hii ya Kikanda na Kitaifa ambayo Benki ya Dunia imepanga kuitekeleza kwa
kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa mwaka ujao wa fedha itahakikisha
kunakuwa na mazingira endelevu na tija kwa kuwa inagusa nchi zote zinazozunguka
maziwa hayo mawili’, alieleza Dkt. Mpango.
Amesema
kuwa ni lazima kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira kadri
iwezekanavyo ili kuendelea kufaidi rasilimali za maziwa hayo makubwa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na nchi jirani
zinazozunguka maziwa hayo.
Aidha
amebainisha kuwa mwakani, Benki ya Dunia imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili
ya tekeleza mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji eneo la Ruhuji ambapo
utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 300.
‘Eneo
hili la sekta ya umeme ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya viwanda kwa
kuwa uchumi wa viwanda hauwezi kukua bila kuwepo umeme wa uhakika’ alifafanua
Waziri Mpango.
Vilevile
Benki ya Dunia (WB) imekubali kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo katika uchambuzi
wa miradi mbalimbali ili kusaidia Serikali ya Tanzania kutokuingia kwenye
madeni makubwa zaidi ambayo hayawezi kulipika.
Waziri
Mpango alieleza kuwa kutokuwa na ufanisi wa kutosha katika kuchambua miradi
ambayo inagharamiwa na fedha za mikopo inasababisha nchi kubeba mzigo mkubwa wa
madeni hivyo ni vyema Tanzania ikahakikisha kuwa miradi hasa ile inayogharamiwa
kwa fedha za mikopo inachambuliwa vizuri ili mradi husika unapokamilika uweze
kulipa deni.
Amesema
kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali itakua na miradi mingi ya kutekeleza,
miongoni mwa miradi hiyo ni kupambana na tatizo la utapiamlo hivyo ni vema kama
nchi ikaangalia namna bora ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia katika
utekelezaji wake.
“Kitaalamu
mpaka mwanadamu anapofikisha siku 1000 ni kipindi muhimu sana kinachoamua
maisha ya mwanadamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa na uwezo gani wa kufikiri,
kutokana na hali hiyo mtu ambaye atakua na utapiamlo uwezo wake utakua ni mdogo
zaidi kulinganisha na mtoto aliyepata lishe bora’” alifafanua Dkt. Mpango.
Katika
kutekeleza mradi huo Serikali itafanya kazi na Benki ya Dunia kwa kushirikiana
na Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe ili kuhakikisha kwamba Taifa
linapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la utapiamlo.
Mikutano
hiyo ya mwaka ya kipupwe kati ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Wataalamu wa
Benki ya Dunia imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Tanzania itanufaika
kutokana programu mbalimbali ambazo zitagharamiwa na Benki ya Dunia kwa mikopo
nafuu.
Post a Comment
karibu kwa maoni