Hali
hiyo iliendelea na kumfanya Mchungaji Msigwa kukatishwa mara kadhaa na
wabunge waliokuwa wakiomba mwongozo na wengine kutoa taarifa, jambo
lililofanya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kutumia muda mwingi
kuwatuliza wabunge waliokuwa wakizomea ama kuangua vicheko.
Hali
ya hewa ilianza kuchafuka baada ya Mchungaji Msigwa kusema; “unamchukua
mtu kama Kitila (Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji) unampeleka
kwenye Wizara ya Maji, anakaa ofisini badala ya kuzungumza mambo ya
kumtua mama ndoo ambalo ni wazo zuri, yeye anakazana anataka amjibu
askofu kwa sababu ya mawazo aliyotoa kwamba hakuna demokrsia,”.
Mchungaji
Msigwa alikatishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Injinia
Stella Manyanya, aliyeomba mwongozo akisema mzungumzaji anaingiza jambo
ambalo halipo kwenye mjadala.
“Mheshimiwa tunza heshima yako usiharibu hii ajenda, jikite kwenye ajenda iliyo mezani,” alisema Injinia Manyanya.
Baada
ya Mwenyekiti kumruhusu Msigwa kuendelea kuzungumza, alianza kwa kusema
“haya ndiyo mambo ninayozungumza, dada yangu namheshimu sana na ni
mhandisi lakini anashindwa kuunganisha utawala bora ninaozungumzia na
mifano ninayotoa, hizi ndiyo appointment (uteuzi) ninazozungumzia, yaani
haelewi kabisa”.
Wakati akiendelea kuchangia, ziliendelea kusikika sauti za baadhi ya wabunge wakisema DNA, DNA.
Msigwa
aliendelea kusema; “mtu kama Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti,
anatumia vibaya ofisi ya umma kwa kugawa kadi za CCM na kusema
hatashirikiana na wapinzani huo si utawala bora”.
Baada
ya kauli hiyo, Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini, Vuma Augustino,
aliomba kumpa taarifa Msigwa ambapo alisema Mkuu wa Mkoa ni mjumbe wa
kamati ya CCM ya mkoa hivyo ana haki ya kutimiza wajibu wake.
Msigwa
alimjibu kwa kusema anarudia kuwa hayo ndiyo alikuwa akiyazungumzia, na
kumuita mbunge huyo kuwa kijana mdogo msomi lakini anashindwa
kutofautisha kazi ya Mkuu wa Mkoa na shughuli za CCM na kuongeza kuwa
hiyo ni huzuni hawezi kuelewa.
“Unamchukua
mtu kama Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda), kila
siku anaharibu, alianza madawa ya kulevya….,” sauti za DNA, DNA zilianza
tena na wakati huu zikiwa nyingi zaidi na kumfanya ashindwe kuzungumza.
Mwenyekiti wa kikao hicho, alitumia takribani sekunde 10 kutuliza wabunge.
Msigwa
aliendelea kuzungumza akisema kama suala ni DNA yuko tayari na anaweza
kushughulika vizuri, huku kelele nyingi zikisikika kutoka upande wa CCM.
Baada
ya hapo, Mbunge wa Siha Dk. Godwin Mollel, aliomba kutoa taarifa ambapo
kabla hajasimama kuanza kuzungumza, Msigwa alisikika akimuuliza “kwani
Mollel na wewe unataka kupimwa mbegu,” jambo lililozua kelele zaidi.
Akitoa
taarifa yake, Dk. Mollel alisema wabunge hao wa Chadema wanachangishwa
Sh milioni 75 kwa mwezi lakini wameshindwa kuajiri watu wanne wa
kuwaandalia hotuba zao.
Wakati
akiendelea baadhi ya sauti zilisikika zikisema “Dk. Shika, Dk. Shika”
hali iliyosababisha wabunge wengi zaidi kuangua vicheko.
Baada
ya wabunge kutulia, Dk. Mollel alisema; “mimi siendi kwenye DNA kwa
sababu ni mambo binafsi,” kauli hiyo ilifanya aendelee kuzomewa jambo
lililomkatisha kwa muda na baadaye kuendelea kwa kusema “umesikia mazuzu
na misukule wananizomea.”
Kauli hizo zilifanya wabunge waangue kicheko huku wengine wakisema; “njaa, njaa,”.
Msigwa
alipopewa nafasi ya kuendelea kuzungumza alianza kwa kusema anaomba
kumsaidia Dk. Mollel huku akimuita bidhaa anayenunuliwa kama karanga
barabarani huyu, mwanaume mzima ananunuliwa kama karanga.
“Hotuba
ya Serikali haijaandaliwa na waziri imeandaliwa na timu kubwa, leo
mnataka sisi tuandae kwa dakika moja kwasababu mnaona tunafanya mchezo
hapa, nakupuuza wewe sijui Dokta wa wapi wewe,” alisema Msigwa.
Baada ya kumaliza kumjibu Mollel, aliendelea na mjadala wake akizungumzia ushauri waliotoa kwa serikali juu ya sekta ya madini.
Hata
hivyo, alikatishwa tena na Jackline Ngonyani, aliyeomba kutoa taarifa
akasema “nilitaka kumwambia Msigwa utawala bora anaozungumzia ni suala
la msingi, lakini unapoanza kunyoosha kidole kwa mwenzako vidole,
vingine vinakurudia wewe, angeanza mwenyewe kwenye suala la DNA, Dar es
Salaam ameshaenda na yule inasemekana ni mke wa mtu.”
Msigwa
alipopewa nafasi ya kumjibu alisema “nataka nimwambie Mbunge, mama niko
vizuri sana, kama unataka suala la DNA niko vizuri labda kama unataka
vitu vingine nako niko vizuri.
“Anayetaka
kuja aje tu, kama mnadhani hiyo ni kiki mnapoteza muda, sasa na
Mawaziri wote tutawapima DNA humu ndani si mnataka tupimane, hamna
shida.
“Ninachozungumza
ndiyo haya, tunaacha kuzungumza mambo ya msingi ya nchi, tunazungumza
mambo ya msingi watu wanakufa mnahangaika na DNA yangu,” alisema Msigwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni