0
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ameitaka Serikali kutekeleza agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu kusuasua kwa miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Chenge ametoa kauli hiyo leo Mei 2, bungeni jijini Dodoma baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu ambapo wabunge wengi walisimama ili kuuliza maswali ya nyongeza zaidi katika maswali yanayohusu Wizara ya Nishati.

Amesema serikali inapaswa kufuatilia maelekezo ya Spika kwa kuwa lipo tatizo.

“Juzi Spika alielekeza lakini angalieni wabunge waliosimama humu kuna tatizo! Nadhani serikali ifuatilie maelekezo ya Spika, lipo tatizo haiwezekani.. angalieni, suala la letter of credit (barua ya mikopo) ndiyo linasemwa na wakandarasi wote hazijafunguliwa,  letter of credit ni tatizo,” amesema.

Chenge alitoa maelekezo hayo baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kujibu swali la Mbunge wa Morogoro Mashariki Kusini (CCM), Omar Mgumba aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuvipatia umeme vijiji vilivyorukwa na miradi wa REA III.

Naibu Waziri huyo alisema mafaili yote ya wakandarasi yameshakusanywa na utaratibu wa kufungua barua hizo za mikopo unaendelea sasa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top