0
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umemsimamisha kazi aliyekuwa Katibu wa umoja huo Mkoa wa Arusha, Ezekiel Mollel kwa kutotii agizo la Makao Makuu linalomtaka kuhama na kusababisha mvutano na malumbano yasiyo na tija kwa CCM mkoani Arusha.
Umoja huo umewataka vijana wa UVCCM kutambua kuwa shughuli za uendeshaji wa umoja huo, zinafanyika kwa kufuata taratibu za kikanuni kwa kuzingatia misingi ya nidhamu na utii.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka amewaeleza waandishi wa habari katika ofisi za UVCCM Mkoa baada ya kumaliza mzozo ulioibuka na kusababisha baadhi ya vijana kufunga ofisi wakimkataa Ezekiel asiendelee kubakia mkoani Arusha.
Shaka amesema Agosti 25, mwaka huu makao makuu ilimuandikia barua Mollel kumhamishia Dar es Salaam, lakini cha ajabu kwa muda wote amekuwa akikaidi kuhama kwa sababu zake binafsi.
Amesema, kikao cha Sekretarieti ya Taifa kilichokaa jijini Dar es Salaam, Septemba 14, mwaka huu, kimeamua kumsimamisha kazi katibu huyo na kumtaka ampishe Katibu wa Mkoa mpya, Said Goha aliyehamia Arusha akitoka Lindi.
Alipoulizwa iwapo ni mpango wa kumuondoa ili kuficha ukweli wa ufujaji wa miradi, amesema kuhama kwake hakuwezi kuzuia ukweli usijulikane, kwa kuwa Jumuiya inafanya uchunguzi wa miradi na rasilimali zake pia vyombo vya serikali vimeombwa viingilie sakata hilo ili kupata ukweli wa mambo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top