0
TAASISI ya Tiba na Mifupa ya Fahamu (MOI) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imekabidhiwa miguu ya bandia 600 yenye thamani ya Sh milioni 60 kwa lengo la kuwasaidia watu wenye uhitaji wa viungo hivyo bandia.
Viungo hivyo bandia vilivyotolewa na Taasisi ya Legs 4 Africa ya Uingereza kwa kushirikiana na asasi ya Mohamed Punjani na Watoto Kwanza ilikabidhiwa jana MOI.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa MOI, Jumaa Almasi amesema taasisi hiyo ilikuwa na uhitaji wa viungo hivyo kwa kuwa wapo watu wanaohitaji kuwekewa viungo hivyo vinavyowasaidia kutembea, hivyo vitasaidia kupunguza tatizo hilo.
“Tunashukuru na kuipongeza taasisi hii kwa msaada huu wa viungo, vitawasaidia watoto na watu wazima waliopoteza viungo vyao kwa sababu mbalimbali,” amesema Almasi.
Kwa mujibu wa Almasi, wagonjwa watakaohitaji kuwekewa viungo hivyo watachangia fedha kidogo kwa ajili ya kurekebishwa kwa kuwa imekuja imeshatengenezwa hivyo ili mtu awekewe ni lazima apimwe ili kiungo hicho kimtoshe.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Watoto Kwanza, Janeth Kiwia amesema wataendelea kuisaidia taasisi hiyo ili kuwasaidia watoto wenye uhitaji maalumu waweze kupata viungo hivyo.
Kiwia amesema miguu hiyo inatarajiwa kutumika katika maabara ya kutengeneza viungo bandia ya MOI ili kutengeneza miguu mingine itakayowasaidia Watanzania ambao watakuwa na uhitaji.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top