0
SERIKALI imepanga kujenga kituo cha kitaifa cha michezo nchini ili kutekeleza mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya michezo katika jitihada za kuinua michezo hapa nchini.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alisema kituo hicho (National Sports Complex) kitaleta chachu ya maendeleo ya michezo nchini.

Wambura aliyasema hayo juzi wakati wa ufungaji wa kongamano la siku mbili la michezo lililofanyika katika Kituo cha Michezo cha Filbert Bayi, Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.

Alisema, serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza michezo nchini, katika kuzalisha ajira na kuchangia pato la taifa, ambapo mpango huo wa miaka mitano wa mwaka 2016-2021, unatambua kuwa, Tanzania ipo nyuma katika michezo, hivyo kunahitajika uwekezaji wa makusudi ili kuinua kiwango cha michezo nchini.

Alisema katika kipindi cha utekelezaji, Serikali imepanga kujenga kituo hicho pamoja na kuendelea kuimarisha chuo cha michezo cha Mallya, ili kupata wataalamu wa kutosha wa kutoa mafunzo ya michezo nchini.
Alisema Wizara inaendelea na mchakato wa kuifanyia mapitio sera ya maendeleo ya michezo ya mwaka 1995, ili kuhakikisha inakwenda sambamba na mahitaji ya sasa.
“Wizara imeandaa utaratibu wa kuwawezesha wadau kuelezea mafanikio, changamoto na mapendekezo yatakayoweza kuzingatiwa katika maandalizi ya sera mpya… ”alisema Wambura.
Naye Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema, pamoja na mambo mengine washiriki katika kongamano hilo wamejadili mada mbalimbali na kutoa maazimio kadhaa yatakayosaidia kukua kwa michezo nchini.
Kongamano hilo la siku mbili lilishirikisha viongozi wa zamani na wa sasa wa michezo, viongozi na wanamichezo wastaafu, likidhaminiwa na Kitengo cha Misaada cha Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (Olympic Solidarity) na TOC.
Wadau walioshiriki kongamano hilo wameiomba serikali kuhakikisha maazimio yaliyofikiwa katika kongamano hilo yafanyiwe kazi ili yawe chachu ya maendeleo ya michezo nchini.
Baadhi ya wakongwe wa michezo waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na mkurugenzi wa kwanza wa michezo nchini Khalfa Abdallah, meneja wa kwanza wa Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Chabanga Hassan Dyamwale na mkurugenzi wa zamani wa michezo, Leonard Thadeo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top