0
SERIKALI mkoani Kigoma imekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii nchini za kutokea kwa ajali na kuanguka kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga akizungumza mjini Kigoma jana alisema hakuna ndege yoyote iliyoanguka mjini Kigoma wala sehemu yoyote ya mkoa huo katika siku za karibuni.
Anga alisema katika kujiridhisha na hilo, alitembelea Uwanja wa Ndege wa Kigoma, kuona hali halisi na kwamba amejiridhisha binafsi pasi na kutia shaka kwamba taarifa zinazosambazwa kuwa ni uongo mtupu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema aliwasiliana na uongozi wa ATCL, ambao umemthibitishia kwamba ndege mpya mbili ambazo zimenunuliwa na serikali ziko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam zikiwa salama, hata ndege hiyo inayoonesha aina ya ATR Dash – 8, ipo salama na inafanya safari zake kama kawaida.
“Huo ni uongo wa kutaka kuitia madoa serikali yetu na shirika letu kuonekana kwamba serikali yetu imefanya uamuzi usiofaa kwa kununua ndege hizo mbili, ukweli huo ni uzushi na unapaswa kupuuzwa,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Pamoja na hilo, aliiomba ATCL kutoa taarifa ya kukanusha uvumi huo, lakini pia aliomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuchunguza chanzo cha uvumi huo na kuwachukulia hatua kali waliosambaza uvumi huo kwa nia ya kuichafua serikali.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top