0

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameahidi kuzungumza na mwenzake wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ili kuhakikisha halmashauri zote nchini zinapanga bajeti ya kununua viuadudu katika kupambana na malaria.
Akizungumza baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Mesa kutembelea kiwanda cha kutengeneza viuadudu, Kibaha mkoani Pwani jana, Ummy alisema hatua ya kuzungumza na Waziri wa Tamisemi ni katika kuhakikisha halmashauri zinunue dawa hiyo kwa lengo la kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.
“Tunataka halmashauri zote zitenge bajeti ya kununua viuadudu ili kila wiki ipulizwe kwenye maeneo yao, kwani na kuhakikisha tunatokomeza malaria na kuifanya nchi isiyo na malaria kama ilivyo Cuba,” alisema.

Aliongeza kuwa malaria ni ugonjwa unaosumbua watu wengi na unaifanya serikali kutumia rasilimali fedha nyingi. Alisema takwimu za sasa zinaonesha kuwa takribani Watanzania 14 kati ya 100, wanaugua malaria wakati uwezo ni kutengeneza lita milioni sita kwa mwaka.
Akizungumza kabla ya kukagua kiwanda hicho na kuzungumza na wafanyakazi kutoka Cuba, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mesa aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujenga kiwanda hicho ambacho kitasaidia katika kupambana na malaria nchini na nchi zingine za Bara la Afrika.
“Kiwanda hiki kina umuhimu mkubwa kwa Tanzania si katika nyanja ya afya pekee, bali hata katika kuongeza ajira kwani zaidi ya wafanyakazi zaidi ya 100 wataajiriwa,” alisema Makamu wa Rais aliyekuwa katika ziara ya siku tatu nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk Samwel Nyantahe alisema kiwanda hicho ni cha kipekee Afrika na kina uwezo wa kuzalisha viuadudu kwa ajili ya soko la ndani, Afrika Mashariki na nchi zingine za Afrika. "Faraja iliyopo ni kuwa wenzetu wa Cuba wako tayari kutusaidia katika masoko mengine kwa ajili ya kuuza bidhaa zetu," alisema.
Kiwanda hicho kilichofunguliwa mwaka jana, kinatarajia kuanza uzalishaji mwishoni mwa wiki hii, ikiwa ni siku kadhaa tangu kupata mkopo wa Sh bilioni nne zikizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top