Serikali
imesema itaweka mikakati madhubuti ya kutangaza madini ya Tanzanite nje ya nchi na
kwamba italifanyia kazi kwa nguvu zake zote suala la madini na kuhakiki mwenendo
wa uzalishaji katika machimbo ya madini ya Tanzanite yanayopatikana eneo la
Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara kutokana na suala hilo kuwa na vikwazo
vingi vya kiuendeshaji.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Getini katika eneo la Mirerani wilayani humo ambapo alisisitiza kuwa serikali pia itahakikisha madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania katika eneo la Mirerani yanatangazwa na kujulikana duniani kote na kuwanufaisha wajasiriamali wadogo na wazawa.
Alisema madini ya Tanzanite yanayopatikana pia India yanajulikana zaidi duniani kuliko yanayopatikana Mirerani, Tanzania na kwamba itaangalia upya ya sheria inayoruhusu makampuni ya nje yanayonunua madini hayo katika ulipaji kodi ili halmashauri husika ziweze kupata mapato ya ndani na serikali kupata
mapato kutokana na minada ya madini hayo na uwekezaji.
Alisema imegundulika kuwa sekta ya madini ina matatizo mengi na migongano kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa na upatikanaji wa leseni za makundi hayo ambapo sheria ya madini nchini inasisitiza wachimbaji na wawekezaji kuwa na leseni jambo ambalo alisema litafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kujua wawekezaji wameingiaje katika maeneo hayo, leseni zao zimepatikana wapi na mfumo wa ulipaji kodi wao.
Waziri mkuu alisisitiza kuwa azma ya serikali ni kuona inawainua wajasiriamali wadogo wa machimbo ya madini ikiwa ni pamoja na kuwa na zana bora za uchimbaji kwa kutambulika kisheria na kwamba ili waweze kufanya kazi hizo za uzalishaji ni lazima waondokane na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi ambapo alisema katika eneo la Mirerani pekee maambukizi hayo yako juu kwa asilimia 18.
Aidha aliwataka wazazi na walezi wa watoto waliofikia umri wa kupelekwa shule wanakwenda shule kwa kuwa serikali imefuta michango ya ulinzi, taaluma, bili za umeme, ada na gharama za mitihani zilizokuwa zikigharamiwa awali na makundi hayo ili watoto wengi wakapate elimu ambapo aliwaagiza maafisa elimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo kusimamia kikamilifu agizo hilo hasa katika eneo hilo ambalo watoto wamekuwa wakitumikishwa katika kazi za migodi.
Akiwasilisha taarifa ya wilaya ya Simanjiro mbele ya waziri Mkuu, Mkuu wa wilaya hiyo Mhandisi Zephania Chaula alisema kuwa wachimbaji wa madini hayo ya Tanzanite baadhi yao hawatoi takwimu sahihi za uzalishaji zinazoiwezesha halmashauri kukusanya kodi ya huduma kutokana na utoroshaji wa madini hayo nje ya wilaya na nje ya nchi.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Simanjiro James Ole Milya alipongeza juhudi za serikali ya uongozi wa awamu ya tano katika kujiletea maendeleo ambapo pia alimwomba waziri mkuu
kuimarisha miundo mbinu ya barabara na huduma za kijamii za maji safi na salama ambapo tatizo hilo limekuwa sugu katika wilaya hiyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni