Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameitaka nchi ya Uingereza
kutazama uwezekano wa kufanya biashara na Tanzania kwa kununua bidhaa
zilizoongezwa thamani badala ya hali ya sasa ambapo nchi hiyo imekuwa ikinunua
bidhaa ghafi ilihali ikiingiza nchini bidhaa zake za viwandani.
Dkt. Mpango ameyasema hayo alipokutana na Mjumbe wa Waziri Mkuu wa
Uingereza anayeshughulikia masuala ya Biashara Bw. Lord Hollick ailipo tembelea
Makao Makuu ya Wizara hiyo jijini Dar es salaam.
Amesema Tanzania inataka kuona inauza bidhaa zake zenye thamani
ambazo zitatokana na maendeleo makubwa ya viwanda hapa nchini ikiwa ni Sera ya
nchi kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.
Nchi ya Uingereza imekuwa ikifanya biashara na Tanzania kwa kiasi
kikubwa na takwimu zinaonesha nchi hiyo inaingiza bidhaa zenye thamani mara
nane ya Tanzania jambo ambalo linatakiwa kurekebishwa ili biashara iwe na
manufaa kwa pande zote mbili.
Miongoni mwa bidhaa ghafi ambazo zimekuwa zikisafirishwa kwenda
uingereza ni pamoja na Chai, kahawa na madini ya vito huku Uingereza ikiingiza
bidhaa za viwandani zenye thamani kubwa ikijumuisha mashine (mitambo),vifaa vya
umeme, bidhaa za plastiki na madawa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Waziri Mkuu wa Uingereza anayeshughulikia
Biashara Bw. Lord Hollick amebainisha
nia ya nchi yake kutaka kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika nchi za Afrika
ikiwemo Tanzania baada ya Taifa hilo kuamua kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.
Maeneo ambayo Uingereza inapenda kuwekeza Tanzania ni katika Sekta
ya Kilimo, Nishati ya Umeme na Usafirishaji huku kwa sasa akionesha nia ya ya
nchi yake kuwekeza katika ujenzi wa kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato
katika Makao Makuu ya nchi - Dodoma.
Pia nchi hizo mbili zimekubaliana kuandaa mkutano utakao
wakutanisha Serikali na Sekta Binafsi ya Tanzania kwa upande mmoja na wawekezaji
wakubwa kutoka Uingereza na nchi nyingine za Ulaya ambao utasaidia kukuza
uwekezaji na biashara na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa manufaa ya
wananchi wa Tanzania na nchi hizo za
Ulaya ikiwemo Uingereza.
Post a Comment
karibu kwa maoni