Crystal Palace imeendelea kurudisha matumaini ya kusalia kwenye ligi kuu ya England baada ya kuichapa Arsenal ambayo nayo inahaha kuingia nafasi ya nne baada ya kukumbana na wakati mgumu.
Iwapo Arsenal itashindwa kuingia nafasi nne bora, itakuwa ni mara ya kwanza tokea imeanza kunolewa na Arsene Wenger mwaka 1996.
Palace wameshinda kwa magoli 3-0 katika mchezo uliokuwa wa kusisimua.
Palace walianza kuongoza kupitia kwa Andros Townsend kisha dakika chache baadaye Yohan Cabaye akapachika goli la pili.
Luka Milivojevic akaiandikia Palace goli la tatu kwa mkwaju wa penalti na kuifanya kuwa alama sita juu ya mstari wa kushuka daraja.
Katika kipindi cha pili Arsenal hawakuweza kupiga shuti lililolenga lango la Palace.
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal waliosafiri kutoka London walibeba mabango yanayomtaka mfaransa huyo kuachia ngazi.
Arsenal ipo alama saba nyuma ya timu ya nne ambayo ni Manchester City ikiwa pia imesalia na michezo nane kabla ya ligi kumalizika.
Post a Comment
karibu kwa maoni